Askari wa Kituo cha Polisi Wilaya ya
Sikonge mkoani Tabora, H 3416 PC Charles, amejiua kwa kujipiga risasi.
Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani
na kituo hicho cha polisi, Paulo Lazaro na Furahisha Felix, walisema tukio hilo
lilitokea Aprili 4, mwaka huu, saa 1:00 usiku kituoni hapo.
“Suala hili limetushangaza, kwani
sisi tulikuwa nyumbani. Ghafla tulisikia mlio wa bunduki katika kituo cha
polisi. Tulipofika, tulimkuta askari huyo akiwa amekufa kwa kujipiga risasi,”
alisema Lazaro.
Wananchi hao walisema kutokana na
hali hiyo, walilazimika kuwauliza baadhi ya askari waliokuwa zamu, ambao
walidai hata wao hawajui ni kwanini mwenzao amechukua uamuzi wa kujiua.
Waliomba ufanyike uchunguzi wa kina
ili kubaini chanzo cha kujiua kwa askari huyo kwani inawezekana kuna kitu
ambacho alikuwa amechukizwa nacho. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana
Kaganda, alithibitisha kujiua kwa askari huyo. “Ni kweli askari huyo amejiua
kwa kujipiga risasi wakati akiwa kituoni majira ya saa 1:00 usiku,” alisema
Kamanda Kaganda.
Hata hivyo, Kamanda Kaganda alisema
hakuna ujumbe wowote ulioachwa na askari huyo kuelezea sababu za kujiua.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Kaganda aliwataka askari wote kutatua matatizo
yao kupitia kwa viongozi wao badala ya kujichukulia sheria mkononi.