Siku chache baada ya baba aliyedaiwa kubaka
watoto wake wawili wakazi wa wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani kutiwa
mbaroni na polisi, mama wa watoto waliokuwa wakitendewa unyama huo ameanza
kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya ndugu wa mume wake.
Mama huyo (jina linahifadhiwa) jana alisema kuwa
baada ya ndugu wa mume wake kupata taarifa ya kukamatwa kwa ndugu yao wameanza
kumtisha ikiwamo ya kutishiwa kuondolewa eneo analoishi na kususiwa
kuhudumiwa watoto wake.
Kutokana na vitisho hivyo mama huyo ameomba
msaada serikalini ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kutokana na vitisho
anavyopokea kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,
Ulrich Matei alisema ofisi yake imepata taarifa za mama huyo kupata vitisho
kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa na kwa sasa jeshi hilo inalifuatilia kwa
karibu zaidi ili kuweza kuwabaini wahusika na watakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo husika.