Tukio hilo la aina yake lilitokea kwenye kwenye majira ya saa moja kasoro za jioni, Jumatano ya April 22, 2015 kwenye eneo maarufu la Mwisho wa lami zilipo ofisi za Chadema wakati chenge na wafuasi wake wakirejea kutoka kwenye mkutano wa hadhara.

“Yaani ni Mungu tu, hivi sasa tungekuwa tunazungumza mengine kuhusu Mheshimiwa Chenge, wafuasi wa Chadema wangemuua,” alisema shuhuda wa tukio hilo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini na kuongeza:
“Unajua siku hiyo kulikuwa na mikutano miwili ya hadhara, mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika eneo la Isanga na kuhutubiwa na Mheshimiwa Chenge na mwingine wa Chadema uliohutubiwa na John Mnyika na Heche.
“Mikutano yote iliisha salama na wafuasi wa Chadema wapatao 2,000, wakawasindikiza viongozi wao kwenda kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami, kandokando ya Barabara ya Maswa- Lamadi,” alisema shuhuda huyo na kuendelea kuongeza kuwa walipofika kwenye ofisi hizo, waliendelea kuimba na kushangilia na kutawanyika mpaka barabarani.
“Ghafla msafara wa Chenge ukafika eneo hilo huku muziki ukisikika kwa sauti kubwa ndani ya gari moja, wafuasi wote wa Chadema wakiwa wameshika mawe wakauzingira na kuanza kuzomea. Mara Chenge na wafuasi wake wakateremka chini, hapo ndipo kiliponuka.
“Mtu mmoja aliwaamrisha wafuasi wa Chadema kuanza kuwapiga mawe watu wote, akiwemo Chenge, kukatokea bonge la mtiti, Chenge na wenzake wakawekwa ‘mtu kati’ na kutaka kushushiwa kichapo.
“Taarifa zilizopo ni kwamba Mheshimiwa Chenge na wenzake walikuwa wakitoka kwenye mkutano halali walioufanya eneo la Isanga, sasa wakati wanarudi wakapita kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami ambapo wafuasi wa Chadema waliwavamia na kusababisha vurugu kubwa.
“Katika kujihami, mtu mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa Chenge aitwaye Ahmed Ismail alifyatua risasi tatu hewani, ndipo wakapata upenyo wa kukimbia baada ya wafuasi wa Chadema kutawanyika.
“Mkanganyiko uliopo ni kwamba CCM wanasema Chadema ndiyo waliowavamia, Chadema nao wanasema CCM ndiyo waliowavamia, hivyo hali ni tete. Tunaendelea kulichunguza tukio hilo,” alisema Kamanda Gemini na kuongeza:
“Wanasiasa wajifunze kupambana kwa hoja wawapo kwenye majukwaa ya siasa lakini siyo kupigana kwa mawe au bastola.”
Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kwamba bastola iliyotumika, ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed na kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa.
   Chanzo Uwazi
 
Top