Ajali zimekuwa janga la kitaifa nchini kwetu ambalo kila kukicha linazidi kutanda na kuenea katika maeneo mbalimbali na kuzidi kumaliza wananchi. Ni muda mfupi tu umepita tangu wananchi walivyochinjwa kama kuku kule Iringa baada ya badi kudondokewa na kontena pamoja na ajali nyingine ya basi kule Handeni mkoani Tanga iliyoua watu 10.

Janga hilo limeendelea kunyanyasa taifa letu baada ya watu 18 kufariki dunia jana na  wengine 11  kujeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Nganga kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso na kulipuka moto.

Tukio hilo lilitokea jana eneo la kijiji cha Msimba, tarafa ya Mikumi, barabara kuu ya Morogoro – Iringa. 

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku mbili tu baada ya madereva kuitisha mgomo nchi nzima kupinga utaratibu mpya uliotolewa na 

serikali uliowataka kwenda kusoma katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kupata utaalamu na kuzijua vizuri sheria za 

usalama barabarani kupunguza ajali.

Hata hivyo, kutokana na mgomo huo ambao ulileta athari kiuchumi na kusababisha kero kwa wananchi, serikali kupitia Waziri wa 

Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ililazimika kuondoa utaratibu huo.

Mbali ya kupinga kutakiwa kusoma, malalamiko mengine ya madereva ilikuwa ni kukerwa na tochi za barabarani ambzo ni maalum 

kwa ajili ya kudhibiti mwendo kasi wa madereva na kutopewa mikataba ya ajira katika makampuni wanayofanyia kazi.

Ajali ya jana ilihusisha basi la Kampuni ya Nganga lenye namba za usajili T 373 DAH aina ya Scania lilokuwa likitokea wilayani 

Kilombero, Morogoro kuelekea mkoani Mbeya na lilipofika katika kijiji cha Msimba likagongana na Fuso namba T 164 BKG 

lilokuwa likitokea Iringa kuelekea jijini Dar es Salaam.

KAULI YA RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo saa 2: 00 asubuhi na kwamba chanzo 

cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Nganga ambaye alikuwa katika mwendo kasi kutaka kulipita gari lilokuwa mbele yake bila ya 

tahadhari na kugongana na lori hilo uso kwa uso.

ABIRIA WATEKETEA MOTO
Kamanda Paul alisema kwa kuwa ndani ya buti ya basi kulikuwa kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta, baada ya magari 

hayo kugongana, ulitokea mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na lori kuwaka moto.

Alisema kuwa kutokana na moto huo, baadhi ya abiria waliokuwamo katika basi walishindwa kujiokoa, hivyo miili yao kuteketea 

kabisa wakiwamo madereva wa magari hayo.

Alisema majeruhi 11 wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito  iliyopo tarafa ya Mikumi ambako 

wanaendelea kupatiwa matibabu, huku baadhi yao hali zao zikiwa mbaya  kutokana na kuungua kwa moto.
Alisema miili ya waliofariki nayo imehifadhiwa katika hospitali hiyo na hadi jana jioni ilikuwa haijatambuliwa majina.

MGANGA AZUNGUMZA

Kwa upande wake, Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu  Kizito, Dk. Boniventure Buyagabuyaga, alithibisha kupokea miili ya 

marehemu 18 ambayo ilikuwa imeteketea vibaya kwa moto na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

Dk. Buyagabuyaga alisema majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika hospitali hiyo ni saba, huku wengine wakiwa wamepelekwa 

katika zahanati ya Mtandika iliyopo kijiji cha Msimba.

AJALI YA ALHAMISI
Ajali hiyo imetokea takribani siku tatu baada ya kutokea ajali nyingine mbili za barabarani zilizoua watu 12 na kujeruhi zaidi ya 80.

Alhamisi iliyopita watu 10 walifariki na wengine 35 kujeruhiwa, baadhi yao vibaya katika ajali iliyohusisha mabasi matatu ya Ratco, 

Ngorika na gari dogo katika maeneo ya Mbwewe, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Ajali nyingine ilitokea siku hiyo hiyo jioni eneo la  Kikwaza, Mikumi, mkoani Morogoro na kuua watu wawili na wengine 48.

Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Happy Nation lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya na chanzo cha ajali hiyo 

kilidaiwa kuwa ni mwendo kasi na kusababisha ligonge nguzo mbili za umeme.

 
Top