Kwa mujibu wa habari hiyo, Muuguzi aliyekuwa zamu aliamua kumchapa viboko mjamzito huyo baada ya kumuona anashindwa kujikamua ili kumsukuma mtoto atoke na alikuwa akifanya hayo akidai kuwa mwanamke huyo ni mzembe na anadeka ndio maana alikuwa anashindwa kujifungua.
Wauguzi wakijadili jambo
Katika toleo letu la jana kulikuwa na habari iliyomuhusu mwanamke mmoja wa
Dodoma ambaye alikuwa amepelekwa kituo cha afya cha Muungano wilayani Chamwino
kwa ajili ya kujifungua, lakini akakutana na vitendo vya kikatili
vilivyochangia mtoto afie tumboni.
Kwa mujibu wa habari hiyo, muuguzi aliyekuwa zamu siku hiyo aliamua kumchapa
viboko mjamzito huyo baada ya kumuona anashindwa kujikakamua ili kumsukuma
mtoto atoke na alikuwa akifanya hayo akidai kuwa mwanamke huyo ni mzembe na
anadeka ndio maana alikuwa anashindwa kujifungua.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikiri kuwapo kwa taarifa za
mama huyo kuchapwa viboko akiwa chumba cha kujifungulia na kwamba wameagiza
uchunguzi ufanyike ili kupata taarifa sahihi za tukio hilo na hatua
zichukuliwe.
Wakati uchunguzi huo ukifanyika, hatutaki kuamini kuwa kifo cha mtoto huyo
kimesababishwa na kupigwa kwa mama yake, lakini kinachotushangaza ni jinsi mama
huyo alivyoshughulikiwa hadi kupoteza kiumbe hicho alichokitunza tumboni kwa
miezi tisa.
Muuguzi huyo ni mmoja tu kati ya wengi ambao wamekuwa wakiwafanyia vitendo
visivyo sahihi wagonjwa wanapoenda hospitalini kwa ajili ya kupata tiba, hasa
wajawazito ambao hulundikiwa mzigo wa maneno kuanzia wanapofika hadi
wanapojifungua. Imekuwa ni kawaida kwa kina mama wajawazito kusimangwa,
kutolewa maneno machafu na kucheleweshewa huduma na matokeo yake baadhi
hujikuta wakipoteza watoto na wengine kulazimika kujifungua kwa kufanyiwa
upasuaji.
Wengine wamekuwa wakilalamika kuwa wauguzi huwaomba rushwa na wasipotoa,
hufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na kudhalilisha.
Mambo hayo husababisha wanawazito wanaoishi kwenye maeneo ya nje ya miji,
kuona ni heri kujifungulia majumbani au kwa waganga wa jadi ambako wanaona
hakuna unyanyasaji kama wanaofanyiwa hospitalini na matokeo yake hukumbana na
athari kubwa zaidi.
Tunatambua kuwa wauguzi wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na
Serikali kutotenga fedha za kutosha kwenye sekta hiyo, lakini hatuamini kuwa
hali hiyo ndiyo inayosababisha wauguzi wafanye vitendo vya unyanyasaji kwa
wagonjwa, na hasa wajawazito.
Tunaamini kuwa katika mazingira hayo magumu, bado wauguzi wanaweza kuonyesha
moyo wa upendo, kufanya kazi kwa weledi na maadili angalau kwa kiwango
kinacholingana na mazingira waliyonayo ili juhudi za kuhimiza kina mama
wajifungulie hospitalini au kwenye vituo vya afya zizae matunda.
Itakuwa ni kitu cha ajabu kama Serikali inapiga kelele kuhimiza wananchi
kwenda kwenye vituo vya afya au hospitalini wakati wauguzi nao wanafanya
vitendo ambavyo vinakatisha tamaa wananchi kwenda sehemu hizo.
Wakati mama huyo akiendelea kupata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa ya
Dodoma, ni vizuri kwa uongozi wa mkoa kufanya uchunguzi wa kina kama
ulivyoahidi ili kupata taarifa sahihi za tukio hilo lililotokea Aprili 3 mwaka
huu, takriban siku 20 zilizopita.
Imekuwa ni kawaida kwamba tukio lolote baya likiripotiwa na vyombo vya
habari, wahusika huwa wepesi kusema wanafuatilia kupata taarifa kamili na
wanapoona hali imepoa, nao wanachana nalo na hakuna hatua zinazochukuliwa.
Matokeo yake ni vitendo hivyo kuendelea kuwa sugu.
Hatutarajii kwamba uongozi wa mkoa wa Dodoma utaingia kwenye mkumbo huo wa
kusubiri hali ipoe, bali utatekeleza ahadi yake ya kufanyia kazi taarifa hizo
ili wahusika wachukuliwe hatua.
Na kwa kuwa huduma duni ni tatizo sugu hospitalini na kwenye vituo vya afya
na hospitalini, Serikali haina budi kufuatilia vitendo hivyo ili kuvikomesha.
Chanzo Mwananchi