Watu 43 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa, huku watuhumiwa 13 wamehukumiwa kunyongwa hadi hufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya watu hao.
Mmmoja wa Albino aliyefanyiwa Ukatili
Waziri mkuu, Mizengo Pinda,
aliliambia Bunge jana wakati akiwasilisha hotuba ya muelekeo wa kazi za
Serikali, makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa
mwaka 2015/16 kuwa, mauaji hayo yamesababisha hofu kwa watu wenye ulemavu wa
ngozi pamoja na familia zao kuishi kwa hofu, mashaka na kushindwa kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Vitendo hivi vimeleta taswira isiyo
nzuri kwa nchi yetu ikizingatiwa kwamba watu wengi ndani na nje ya nchi
wanafahamu kuwa Watanzania wanaishi kwa upendo, kuheshimiana na kuthamini
amani, jambo ambalo nchi nyingi zinaendelea kuiga,” alisema.
Alisema tangu mauaji hayo yalipoanza
mwaka 2006, watuhumiwa 181 walikamatwa na kuhojiwa na kwamba kati ya yao 131
walifikishwa mahakamani, ambapo 46 walifunguliwa kesi za kuua na kujeruhi na
kwamba kati yao washtakiwa 13 wamehukumiwa kifo.
Aidha, mshtakiwa mmoja alihukumiwa
kifungo cha miaka 20 kwa hatia ya kujeruhi, wakati wengine 73 wameachiwa huru
baada ya kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani.
Kutokana na hali hiyo, Pinda alisema
kuanzia mwaka 2006 hadi sasa watu 43 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa, huku
mwaka huu pekee wakiwa wameuawa watu tisa.
Alisema watuhumiwa sita
hawajakamatwa na upelelezi wa kesi 10 bado unaendelea, huku watuhumiwa wawili
wakiuawa na wananchi kabla ya kufikishwa polisi. Pinda alisema chanzo kikubwa
cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwa tamaa za kupata utajiri au chezo.
“Mimi siamini kwamba cheo, wadhifa, mali au utajiri hupatikana kwa njia haramu
kama hizo.
Utajiri hupatikana kwa kufanyakazi
kwa juhudi na maarifa na siyo vinginevyo…serikali itaendelea kupambana na watu
wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa nguvu zake zote,” alisema. Awali,
akizungumza bungeni kabla ya kutoa hutuba, Pinda alisema Kanda ya Ziwa
inaongoza kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ambapo kati ya watu 43
waliouawa 41 wametoka katika kanda hiyo.
Ufafanuzi huo alitoa wakati
alipokuwa akitoa majibu ya ziada katika swali la msingi lililoulizwa na Mbunge
wa Viti Maalum, Martha Umbulla (CCM), ambaye alitaka kujua sababu za
mauaji ya albino kuendelea licha ya kwamba kumekuwa na juhudi za kukomesha vitendo
hivyo.
Alisema ili kuelimisha na
kuhamasisha wananchi wa mikoa hiyo ikiwamo Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga,
Kagera na Mara kuacha imani hizo za kishirikina, Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora (CHRAGG) pamoja na viongozi wa dini watatembelea
na kuhamasisha wananchi wa ameneo hayo kubadili tabia. Aliliambia Bunge kuwa
tume hiyo ya haki za binadamu na madhehebu ya dini yatatembelea kanda
hiyo na kuzungumza na wananchi na kutoa elimu inayolenga kuleta
mabadiliko. Alisema serikali ina amini kuwa kampeni hiyo pamoja kazi za
mahakama itapunguza mauaji ya albino nchini.
Vitendo vya kuwakata viungo albino
vilianza 2006 kwa imani potofu kuwa ni chanzo cha utajiri , mafanikio kisiasa
na kiuchumi. Baadhi wanaamini kuwa vinasaidia kupanda vyeo na kufanikiwa
kazini.
Chanzo Nipashe