Serikali imefuta hatimiliki ya shamba la mkonge la Kikwetu, mkoani Lindi baada ya mmiliki wake kampuni ya Amboni Estates Ltd, kushindwa kuliendeleza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa manispaa hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Ilulu mjini hapa juzi.
Shamba hilo linalodaiwa kupewa hati ya umiliki wa miaka 99 na baadaye kampuni ya Tasco kabla ya kuchukuliwa na Mohamed Enterprieses Tanzania Ltd lilikuwa likizalisha mkonge kwa ajili ya kutengeneza magunia na bidhaa zingine.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kupitia mamlaka aliyopewa kisheria, Rais Magufuli (pichani) amefuta leseni ya umiliki wa shamba hilo na kuwa chini ya serikali.
Majaliwa alisema tayari shamba hilo lipo huru na kampuni ya BSG ipo huru kujenga mitambo itakayotumika kusafishia gesi asilia kwenye eneo hilo.
Kuhusu uendelezwaji wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Meis ambacho ujenzi wake umesimama kwa muda kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kisiasa, Majaliwa alisema kazi hiyo inatarajiwa kuanza tena muda mfupi ujao baada ya kupatikana kwa wataalam.
Alisema kujengwa kwa viwanda ndani ya mji huo, kutasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.
Shamba la mkonge la Kikwetu lililopo ndani ya Manispaa ya Lindi awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya Amboni Estates Ltd halafu Tasco na baadaye Mohamed Enterprieses Tanzania Ltd ya jijini Dar es salaam.
CHANZO: NIPASHE