Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Rainata Mzinga
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Issa Mfaume (31), mkazi wa Likongowele Mkoani Lindi amefikwa na mauti baada ya kutoroshwa kituoni na kupigwa kisha kuchoma moto.

Lindi: Kundi la watu wasiofahamika wakiwa na pikipiki walivamia kituo cha Polisi cha Lionja na kumtorosha bwana Mfaume ambaye alikuwa ameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya Zalali Lunje kwa kumchoma kisu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Watu hao waliwazidi nguvu askari na kufanikiwa kuondoka na mtuhumiwa huyo. Walimpeleka sehemu ambayo inasadikiwa kuwa alimchoma kisu Zalali na kumsababishia mauti. Walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwilini na walipoona ameishiwa nguvu kabisa wakamchoma moto hadi mtu huyo kufikwa na mauti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Rainata Mzinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi, karibu na Kituo cha Mabasi cha Liwale.

Kamanda Mzinga amesema kuwa Jeshi la polisi linawatafuta wahusika wa tukio hilo ili kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kujichukulia sheria mkononi.
 
Top