Waziri wa Nishati na
Madini, Prof Sospeter Muhongo
Akiwasilisha maelezo
ya Serikali leo, Prof Muhongo alipangua hoja moja baada ya nyingine
zilizotolewa na Kamati ya PAC jana na kusisitiza kuwa fedha hizo si mali ya
umma.
Dodoma. Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow linaendelea kuchukua sura mpya baada ya Waziri wa Nishati na
Madini, Prof Sospeter Muhongo kutoa ufafanuzi wa Serikali bungeni mjini Dodoma
kuwa fedha hizo si za umma na kwamba bado Serikali ina mzigo wa madeni katika
sakata hilo.
Kauli ya Prof Muhongo inakuja siku moja baada ya Kamati ya PAC kuwasilisha
ripoti yake jana juu ya suala hilo ambapo pamoja na mambo mengine, Kamati ya
PAC ilijiridhisha kuwa sehemu ya fedha hizo ni za Serikali.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akisoma taarifa ya kamati hiyo jana alisema
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Francis
Mwakapalila, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade wakithibitisha kuwa sehemu ya
fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa za Serikali.
Akiwasilisha maelezo ya Serikali leo, Prof Muhongo alipangua hoja moja baada
ya nyingine zilizotolewa na Kamati ya PAC jana na kusisitiza kuwa fedha hizo si
mali ya umma.
Prof Muhongo pia alitumia muda mwingi kueleza jinsi Kampuni ya uwakili ya
Mkono and Advocates iliyokuwa ikiitetea Serikali pamoja na Tanesco, ilivyochota
kiasi kikubwa cha pesa kama malipo ya kazi hiyo tangu kuanza kwa mgogoro huo.
“Gharama za mawakili; Kampuni ya Mkono & Advocates waliokuwa wakiitetea
Tanesco na Serikali katika suala la IPTL tangu mwaka 1998 hadi 2013 ni Sh62.90
bilioni na bado wanaidai Serikali $ milioni nne,” alismea Prof Muhongo.
Aliongeza kuwa Kampuni hiyo ya Mkono & Advocates iliishauri Serikali
kuwapa kazi nyingine ya kwenda kuitetea Serikali juu ya mgogoro huo, lakini
Serikali ilikataa na kuongeza kuwa waliokoa Sh95 bilioni kwa uamuzi huo kwani
uwezekano wa kushinda ulikuwa mdogo.