Mussa Hassan Mgosi
Mgosi ameisaidia Mtibwa Sugar kuongoza
katika ligi msimu huu.
Dar es Salaam. Mshambuliaji mahiri wa Mtibwa Sugar, Musa Hassan ‘Mgosi’
ameitaka klabu yake ya zamani ya Simba kuvunja benki kama kweli ina nia ya
dhati ya kupata saini yake kwenye kipindi hiki cha usajili.
Masharti hayo ya Mgosi ameyatoa baada ya taarifa zilizoenea kuwa Simba ina
mpango wa kumrudisha mshambuliaji huyo ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji
ambayo imepoteza makali yake tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ikiwa imepachika
mabao saba tofauti na misimu iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mgosi alisema anafahamu heshima aliyonayo
mbele ya viongozi, mashabiki na wapenzi wa Simba ila kama kweli wana nia ya
dhati ya kumsajili wanatakiwa waandae fungu kubwa la pesa ili kumng’oa kwenye
kikosi cha Mtibwa kwani anategemea soka kuendesha maisha yake.
“Ni kweli kuna viongozi wa Simba wameonyesha nia ya kunisajili kwenye
dirisha hili dogo la usajili, lakini tayari nimeshawaambia kuwa nina mkataba na
timu yangu, hivyo wanatakiwa wazungumze na uongozi wa Mtibwa na kumalizana nao
kabla ya kufanya mazungumzo na mimi.
“Pia nimewaambia kuwa wanatakiwa waandae dau nono ambalo pengine litanifanya
niwe mchezaji ghali nchini.
“Nimewaweka wazi kuwa napata maslahi mazuri Mtibwa Sugar na hivyo si rahisi
kunishawishi niondoke hapa kwa sasa kwenda kwao kwa dau dogo, hilo kamwe ziwezi
kulifanya, naiheshimu lakini hii ni ajira,” alisema Mgosi.
MWANANCHI