Mwenyekiti wa Mtaa wa Forodhani
Sirari, Nyangoko Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mkazi wa Kitongoji cha Nyamorege
kilichopo Mtaa wa Forodhani mji mdogo wa Sirari Wilaya ya Tarime mkoani
Mara, Marwa Kihiri Mwita, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma
za kumuua baba yake mzazi Kihiri Mwita kinyama kwa kumpiga na koleo
kichwani na ubavuni.
Vilevile inadaiwa kuwa mtuhumiwa
huyo alijeruhiwa kwa kucharangwa kwa panga na baba yake huyo kabla ya kumjeruhi
kwa kumpiga na koleo kichwani na ubavuni baada ya kuzuka ugomvi baina yao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Forodhani
Sirari, Nyangoko Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Ijumaa
ya wiki iliyopita jioni katika kitongoji hicho.
Paulo alisema kuwa ugomvi huo
uliibuka baada ya baba kumtuhumu mwanaye kuwa anatabia ya wizi.
Alisema inadaiwa kuwa baba huyo
alimweleza mwanaye huyo kuwa aliwahi kufanya wizi kitendo kilichosababisha
kutozwa faini ya ng'ombe.
Paulo alisema inadaiwa kuwa baada ya
baba kutoa tuhuma hizo, mwanaye alitoroka na kuwa nje ya familia kwa zaidi ya
miaka mitano.
Alisema aliporudi nyumbani kwao,
baba alikerwa na kuanza kumfukuza kwa panga ili asiingie ndani kwake huku
akisisitiza aende akaishi kwa wahalifu wenzake.
Mwenyekiti alisema baba akirusha
panga na kumkata mkononi, mwanawe alichukua koleo na kumpiga nalo kichwani na
ubavuni.
Alisema majirani walijitokeza kumuokoa
na kuwakimbiza Hospitali ya Wilaya Tarime ambako alikufa kabla ya kuanza
kupatiwa matibabu.
Polisi Tarime Rorya
wamethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa
mahojiano kisha atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.