- Yadai ni lazima Kumsajili Hata kama baba yake hayupo tayari.
Uongozi wa Simba umeyapuuza maneno yaliyotolewa hivi karibuni na baba mzazi wa Simon Msuva, Happygod Msuva aliyoyatoa hivi karibuni baada ya uongozi wa klabu hiyo kudai kuwa utahakikisha unamnasa.
Hivi karibuni uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili,
Zacharia Hans Pope, ulitangaza kuwa una mpango wa kutaka kumsajili nyota huyo
ambaye hivi karibuni alionyesha kiwango kikubwa akiwa na klabu yake ya Yanga na
kuisaidia kuibuka na ushindi kwenye mechi nne kati ya saba.
Baada ya kauli hiyo ya Simba, mzee Happygod aliliambia gazeti hili kuwa,
anawashangaa viongozi hao kwa hatua hiyo waliyofikia kwani hapo awali kabla ya
mwanaye kuwa na jina kubwa, waliwahi kumkataa na ndipo alipoamua kwenda Yanga.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Simba, Humphrey Nyansio,
alisema kuwa, maneno hayo ya mzee Happygod hayajawakatisha tamaa na hivyo bado
wanaendelea na mpango wao huo.
Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutaka kuonana na uongozi wa Yanga ili kuzungumza nao juu ya mchezaji huyo na baada ya hapo watakaa na Msuva mwenyewe.
“Maneno hayo ya baba yake Msuva hayawezi kutukatisha tamaa eti tuachane na
mpango wetu huo, mikakati yetu ni kuhakikisha tunamsajili mchezaji huo ili kuiongezea
nguvu safu yetu ya ushambuliaji,” alisema Nyasio.
Msuva hivi sasa yupo na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho kipo
nchini Swaziland kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa na timu ya taifa
ya nchi hiyo itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Somhlolo nchini humo
Source Global Publisher