Balozi Sefue amemsimamisha kazi Ndugu Maswi kuanzia , Jumanne, Desemba 23,
2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa
Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema
kuwa amechukua hatua hiyo “Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya
Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)”ambapo “Katibu
Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na
Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Badala yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati
na Madini, Mhandisi Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya
Nishati na Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi
utakapokamilika.Taarifa hiyo ya Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais
Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa jana, Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako
Rais alisema:
“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa
Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza
Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za
kinidhamu zitachukuliwa.”
Ndugu Maswi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na
Mawaziri wawili walituhumiwa wakati wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na
Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati huo huo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine
zinazochukuliwa, Shirika la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL
kuhusu uwezekano wa kushusha tozo la uwekezaji (capacity charge) zaidi ya
punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha
Migogoro ya Kimataifa
Chanzo: BBC
Chanzo: BBC