“Kuna suala la escrow, zamani kulikuwa na aspro ambayo ilikuwa ni dawa ya kweli, sasa suala hili limefikia tamati hamkunichagua ili nikawe waziri, ni sawa na kusema Bwana alitoa na Bwana ametwaa,” alisema Profesa Tibaijuka.
Muleba. Siku moja baada ya kufukuzwa uwaziri, Mbunge
wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amewasili jimboni kwake na
kusema, “Bwana alitoa na Bwana ametwaa.”
Profesa Tibaijuka alivuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
na Rais Jakaya Kikwete juzi kutokana na kuhusika kupokea fedha katika akaunti
binafsi.
Baada ya kuwasili na kupokewa kwa maandamano, Profesa Tibaijuka aliwaomba
wananchi kukaa kimya kwa dakika moja ili kumkumbuka katibu wake wa jimbo
aliyefariki dunia wakati sakata hilo likijadiliwa bungeni.
Profesa Tibaijuka aliyepokewa kwa msafara wa magari kutoka Uwanja wa Ndege
wa Bukoba, aliwaeleza wananchi kuwa ilikuwa ni lazima kutafuta msaada kwa watu
wengi ili aweze kuwasomesha watoto anaowasaidia kielimu.
“Kuna suala la escrow, zamani kulikuwa na aspro ambayo ilikuwa ni dawa ya
kweli, sasa suala hili limefikia tamati hamkunichagua ili nikawe waziri, ni
sawa na kusema Bwana alitoa na Bwana ametwaa,” alisema Profesa Tibaijuka.
Aliambatana na mtoto wa kike akisema ni mmoja wapo wa wanafunzi wasio na
uwezo anaowasomesha katika Shule ya Babro Johanson, inayotajwa kuwa ndiyo
iliyopokea Sh1.6 bilioni alizoingiziwa katika akaunti yake binafsi, katika
Benki ya Mkombozi.
Profesa Tibaijuka alitumia muda mfupi kuelezea suala la kuhusishwa katika
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow akisema Taifa lina changamoto ya kupata
elimu bora na wapo viongozi wachache kama yeye wenye moyo wa kusaidia masuala
ya elimu.
“Teknolojia sasa imekua, naamini mlikuwa mnafuatilia mambo yalivyokuwa
yanakwenda, yalikuwa ni mambo makubwa, kazi ya uwaziri nisingeipata bila nyinyi
wananchi. Nilikuwa na majukumu mengi, sasa nitapata muda wa kukaa jimboni.
“Taifa bado lina changamoto ya kupata elimu bora, hiyo shule mnayoisikia ada
yake kwa mwaka ni zaidi ya Sh4 milioni, hivyo lazima nitafute mtu wa
kunisaidia. Hakuna mtoto wangu hata mmoja anayesoma kwenye shule hizo,”
alisema Tibaijuka.
Huku hotuba yake ikikatizwa na watu waliokuwa wakishangilia, Profesa
Tibaijuka aliwaonya wanaotaka kulinyemelea jimbo hilo kuwa yuko ‘fiti’ na
anawasubiri kukutana nao ulingoni.
Alisema atakuwa tayari kufanya kazi katika maeneo yanayoongozwa na vyama vya
upinzani jimboni kwake akiamini kuwa pia wapo wanachama wa CCM.
Crdt: Mwananchi