Azitaja baadhi yake zinazofanyiwa kazi kuwa ni pamoja na ile
ya Bandari, Bodi ya sukari na ile ya ubinafsishaji wa Benki ya NBC.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kabwe Zitto amesema baada ya kukamilisha shughuli ya ufisadi wa
Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo Sh306 bilioni zilichotwa, kamati yake sasa
inaelekeza nguvu katika kashfa nyingine nne.
Zitto alisema kamati yake itatumia mwezi huu na Januari kupitia ripoti nne
ambazo zina masilahi kwa Taifa, ikiwamo ya utoaji wa vibali vya kuagiza na
kuingiza sukari nchini.
Alisema ufisadi katika utoaji wa vibali hivyo ni mkubwa kuliko sakata la
escrow... “Hili linagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, wamiliki wa viwanda
na uzalishaji. Tayari tumewaita Bodi ya Sukari tujadiliane kwa kina kuhusu
suala hili,” alisema.
Mbali na suala la sukari, alizitaja ripoti nyingine kuwa ni ya uchunguzi wa
ubinafsishaji wa Benki ya NBC, ripoti maalumu ya Bandari na mikataba ya gesi.
“Baada ya kazi ya PAC, tunapumzika, kwani kama unavyojua kazi ilikuwa ngumu,
wiki mbili nilikuwa silali. Kwa kuwa tuna ratiba ya wiki mbili. Kwa Desemba na
Januari tutaanza kuzifanyia kazi,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (Chadema).
Wiki iliyopita, Bunge lilijadili ripoti ya PAC kuhusu ufisadi katika Akaunti
ya Tegeta Escrow na kuhitimishwa kwa kuweka maazimio manane yakiwamo ya kuitaka
Serikali iwawajibishe baadhi ya mawaziri na watendaji wengine wakuu huku
likitaka pia uchunguzi uendelee kwa wote waliotuhumiwa kupokea fedha hizo kwa
njia moja au nyingine.
Kauli ya Zitto inakuja wiki moja baada ya wamiliki wa viwanda vya sukari vya
Kagera, Mtibwa na Kilombero kutishia kuvifunga kutokana na kuviendesha kwa
hasara.
Wamiliki hao walisema watafunga viwanda hivyo kutokana na Serikali kushindwa
kuzuia uagizwaji wa sukari nchini kinyume cha taratibu.
Mkurugenzi wa Viwanda vya Kagera na Mtibwa, Seif Seif alisema uagizaji wa
sukari kutoka nje unafanyika kwa ushirikiano wa wafanyabiashara wakubwa na
vigogo serikalini kinyume cha makubaliano na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya
viwanda.
“Tulikubaliana kwamba Serikali iwe inaagiza tani 100,000 kutoka nje lakini
sukari inayoingizwa sokoni ni zaidi ya tani hizo. Sukari tunayozalisha katika
viwanda vyetu ipo na haina pa kwenda,” alisema Seif na kuongeza:
“Leo ukipita katika maduka utakutana na sukari ya kila aina, wafanyabiashara
wanaoagiza wanawatumia vigogo serikalini kuingiza sukari wapendavyo, tena bila
kulipa kodi,” alisema Seif.
Kutokana na hali hiyo, Seif alisema wamelazimika kupunguza wafanyakazi 2,000
na kubakiwa na 5,000 katika Kiwanda cha Kagera, Kilombero imepunguza 3,000 na
wamebaki 6,000 huku Mtibwa ikiondoa wafanyakazi 3,000.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari Kilombero, Balozi Ami Mpungwe alisema: “Hali ni mbaya, tunaona kuliko kuendelea na hali hii ni bora tusimame kuzalisha sukari.
“Serikali kama kweli ina dhamira ya kuvifufua na kuviendeleza viwanda vyetu vya ndani ni lazima kuvilinda na kupiga marufuku uagizwaji holela wa sukari kutoka nje.”
CHANZO: MWANANCHI