Wasichana wawili mkoani Mara Bhoke Mwita Gisiri (16) na Matinde Kimoto wambura (16) wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Corolla yenye namba za usajili T 388 AGV Katika kijiji cha Msege, kata ya Nyarukoba, tarafa ya Ingwe wilayani Tarime.


Ndugu wa Marehemu hao wametelekeza miili ya watoto wao katika hospitali ya wilaya ya Tarime kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutunza mila na desturi.

Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa mila za Wakurya za kipindi hicho, mwanamke aliyekeketwa pindi anapofariki dunia hutupwa kichakani. Hivyo ndugu wa marehemu Bhoke Mwita na Matinde kimoto wametelekeza miili ya mabinti hao kwasababu nao wamekeketwa.

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Tarime/Rolya, Sweetbert Njewile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mnamo Januari 3 mwaka huu, na kueleza kuwa dereva wa gari iliyowagonga alikimbia na anasakwa na jeshi la polisi kwaajili ya kujibu shitaka.

Aidha, miiliya ya wasichana waliofariki dunia kwa ajali hiyo imehifadhiwa kwenye hospitali ya wilaya ya Tarime.
 
Top