Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume  ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba (kulia) akimkabidhi Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (Kushoto) Katiba Inayopendekezwa. Picha ya Maktaba
  Kama ni ndiyo, maana yake yaendelea marekebisho ya Katiba ya sasa na kama ni hapana, maana yake itumike Katiba ya sasa bila marekebisho.
  Kinachovutia zaidi kama kura zote zitasema ‘ndiyo’ basi matokeo ya kura zilizopigwa yatakuwa yameamuliwa kwa misingi ya asilimia 50 ya jumla ya kura zilizopigwa Tanzania Bara na zaidi ya asilimia 50 Zanzibar na Katiba Mpya itakuwa imekubaliwa. Lakini kuna tofauti gani baina ya Katiba Inayopendekezwa na ile ya Mwaka 1977?
Inashangaza sana kusema kuwa  mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaosubiri Kura ya Maoni miezi mitatu ijayo, umeacha mvurugano na mgawanyiko kuliko hapo awali. Muda ndiyo utakaothibitisha ukweli huu na hii haimaanishi hata kidogo kuidharau Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, utata wa kisheria ulionekana katika mchakato mzima umeacha maswali mengi yaliyotakiwa kutafutiwa majibu. Kuna mambo mengi ya kisheria yahusianayo na kura ya maoni ambayo yametuacha katika wakati mgumu kutokana na mgongano wa masuala ya kisheria yanayotegemeana.
Ukichunguza kwa makini mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, bila shaka utaungana nami kuwa kuna mtego na tupo katika wakati mgumu usio wa kawaida. Kabla sijaeleza mtego upo wapi, napenda nieleze maana ya mtego au kipindi cha wakati mgumu kwa Kiingereza “catch 22 situation”.
Nyaraka mbalimbali zinabainisha kuwa Joseph Heller alitumia neno hilo katika riwaya yake mwaka 1961 iliyoitwa “A catch 22.”   Hali hii hutokea pale mtu anapokuwa hawezi kuikimbia kutokana na taratibu au kanuni zinazokinzana.
Catch 22 mara nyingi huzaliwa kutoka katika sheria, kanuni, au taratibu ambazo mtu anatakiwa kuzifuata, lakini hana uwezo wa kudhibiti au kuziongoza kwa sababu kupingana nazo ndiko kukubaliana nazo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 83 ambacho naomba nikitengeneze upya, iwapo kura nyingi zilizopigwa zikasema ‘Hapana’  katika Kura ya Maoni ya Katiba Inaopendekezwa  basi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 itaendelea kutumika.
Kwa maana hiyo, kupitia sheria hii iwapo watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapigia Katiba Inayopendekezwa kura ya hapana basi tutalazimishwa moja kwa moja kurudi katika Katiba ya mwaka 1977.
Kinachovutia zaidi kama kura zote zitasema ‘Ndiyo’ basi matokeo ya kura zilizopigwa yatakuwa yameamuliwa kwa misingi ya asilimia 50 ya jumla ya kura zilizopigwa Tanzania Bara na zaidi ya asilimia 50 Zanzibar na Katiba Mpya itakuwa imekubaliwa. Lakini kuna tofauti gani baina ya Katiba Inayopendekezwa na ile ya Mwaka 1977?
Swali hili ni la msingi siyo tu katika kuonyesha mtego ulipo, lakini pia kupitia misingi isiyokubaliwa na wengi na chama kama Katiba Inayopendekezwa ilivyopitishwa kwa mvutano mzito ambao baadaye ulileta mgawanyiko uliosababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kususia Bunge hilo.
Kwa maoni yangu huu ulikuwa ushahidi tosha wa mgawanyiko siyo tu kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba, bali kwa nchi nzima kutokana na hoja kuwa wajumbe hao walikuwa wakiwakilisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano. Mungu atuepushie mbali!
Hata hivyo, ukweli ni kwamba Katiba Inayopendekezwa imeongeza kitita cha vipengele vipya hususan vinavyohusiana na haki za binadamu katika rasimu ya mwisho na vipo katika Katiba ya mwaka 1977 kwa kufanyiwa mabadiliko kidogo.
Kwa maana hiyo, machaguo yaliyowekwa mezani kwa ajili ya watu kupigia kura wakati wa Kura ya Maoni ni kwamba aidha upigie ‘Ndiyo’ ili tuishie na maboresho ya Katiba ya mwaka 1977 au upigie ‘Hapana’  ili twende kwenye Katiba ya mwaka 1977 bila mabadiliko yoyote. Huu ni mtego.

Watalaamu wanasema kuwa utawala wa sasa unaridhika na matokeo yoyote yatakayotokea baada ya Kura ya Maoni ambayo yatakuwa yakiendelea kulinda masilahi yake. Nasita kujadili ni kitu gani kilienda tofauti kwenye mchakato huo lakini siyo kwa maana ya kuyazika masuala chanya yaliyoibuka.
Elimu ya uraia.
Mchakato huo kwa mtazamo wangu, umechangia sana elimu ya uraia kwa umma. Mchakato pia umeonyesha misimamo ya kisiasa ya Vyama vya Siasa katika masuala mbalimbali pia umesababisha kuzaliwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Tanzania Kwanza, mambo ambayo ni mapya katika uga wa siasa.
Hata hivyo, tofauti na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, upembuzi wa kawaida unaonyesha kuwa Katiba Inayopendekezwa huenda isiliguse kundi kubwa la watu hususan maudhui yake katika kipindi cha miezi mitatu iliyosalia kupigia Kura ya Maoni jambo ambalo ni bahati mbaya. Lakini kama nilivyoeleza hivi karibuni, mazingira ya kuitengeneza Katiba Inayopendekezwa yaliharibiwa na kukosa uhalali wa kisiasa.
Hivyo basi kuna haja ya mamlaka husika na taasisi za kiraia kutumia nafasi zao vizuri katika kuwaelimisha wananchi hususan juu ya maudhui ya Katiba Inayopendekezwa  dhidi ya ile ya mwaka 1977 pia kuelimisha rasimu ile ya Jaji Warioba.
Nafahamu kuwa baadhi ya taasisi kama ya Mfuko wa Mwalimu Julius Nyerere, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) zinajitahidi kufanya kazi hiyo kwa umakini licha ya uhaba wa rasilimali.
Ni muhimu kwa kila NGO kuratibu na kuandaa ajenda kwa kuwa siyo jambo jema kuviachia vyama vya Siasa pekee kuongoza mchakato wa kampeni za kupigia kura Katiba Inayopendekezwa, kwani kuna hatari kubwa kuviachia vyama hivyo viongoze mchakato huo kwa mlendo wa ilani zao.
Mwandishi ni wakili wa Mahakama Kuu, mshauri wa sheria na mwananchama wa TLS. 

 
Top