Akiongozwa na Wakili wa Serikali, George Mbalasa shahidi huyo alieleza kuwa baadaye alifungua kesi yenye namba RB/8684/2013 na IR/4473/2014 kisha alichukua maelezo mafupi yaliyoandikwa na RCO ambaye alikuwa kama mlalamikaji kisha kuyaweka kwenye jalada la kesi hiyo.

Morogoro. Shahidi watatu katika kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda ametoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro huku mawakili wa upande wa mashtaka na wa utetezi wakisigana kwenye kifungu cha 150 hadi 152 cha sheria ya ushahidi.

Pande hizo mbili zilivutana katika kifungu hicho baada ya Wakili wa Upande wa Utetezi, Abubakar Salim kuiomba Mahakama kutoa uamuzi wa kile alichodai kuwa wakili wa upande wa mashitaka ulimuuliza shahidi maswali ya muongozo kupitia maelezo ambayo yalitolewa na shahidi aliyepita bila ya kuiomba ruksa Mahakama.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo shahidi huyo ambaye ni askari polisi mwenye namba F4103 PC Ernest anayefanyakazi kwenye chumba cha mashtaka katika kituo kikubwa cha Polisi Mkoa wa Morogoro aliieleza Mahakama kuwa Agosti 10 alipokea maelezo kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, RCO Jafert Kibona yanayohusu kesi ya uchochozi inayomkabili Sheikh Ponda.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, George Mbalasa shahidi huyo alieleza kuwa baadaye alifungua kesi yenye namba RB/8684/2013 na IR/4473/2014 kisha alichukua maelezo mafupi yaliyoandikwa na RCO ambaye alikuwa kama mlalamikaji kisha kuyaweka kwenye jalada la kesi hiyo.

Wakili wa upande wa utetezi, Juma Nassoro alimuuliza maswali shahidi huyo ili kutaka kujua kama alikuwapo eneo la tukio hata hivyo shahidi huyo alidai hakuwapo eneo hilo.

Top