Ni kuhusu kutumia viungo vya albino, wadai wengi huuawa
mwaka wa uchaguzi
Kilimanjaro. Waganga wa jadi wanaotumia viungo vya watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino) ikiwa ni sehemu ya tiba, wametakiwa kutofanya
hivyo kwa kuwa huo ni ukatili dhidi ya binadamu.
Mwenyekiti wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asili
Kilimanjaro (Chawatiata), Hasani Kabelo alisema hayo kwenye mkutano wa mwaka wa
chama hicho.
Kabelo alisema wanasiasa na wananchi wanatakiwa
kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wanaojihusisha na matukio ya kikatili
kwa albino.
Kabelo alisema ili kukomesha unyanyasaji dhidi ya albino,
ni lazima jamii ielimishwe kurejea katika imani za dini zinazosisitiza
kuthaminiana bila kujali hali na tofauti za kimaumbile.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu,
albino wanawindwa, hivyo ni jukumu la kila mmoja makini ili kuepuka mauaji
dhidi yao.
Katibu wa chama hicho, Fadhila Mohamed aliwataka waganga
na wakunga wa tiba asili kujisajili kwenye chama hicho kinachotambulika.
Alisema kuna baadhi ya waganga wapo kwa masilahi yao
binafsi kwa kupiga ramli na kuwadanganya watu.
Alisema hao ndiyo wanaosababisha waganga waonekane wabaya
mbele ya jamii Pia, alisema kuwa kuna waganga wanaotoka mikoa ya jirani
wanafikia nyumba za wageni na kufanya kazi za uganga kinyemela kisha
wanaondoka.
Aliishauri Serikali kuwakamata waganga hao kwa kuwa wengi
wao ni matapeli.
Jumla ya waganga na wakunga wapatao 50 walihudhuria
mkutano huo.
Chanzo: Mwananchi