Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu asema walikwenda kununua
vifaa vya kufanyia doria
Dodoma. Mhifadhi wa Wanyamapori, George Kimaro na kibarua
Antony Andrew wameuawa kwa kupigwa mawe na wananchi katika Kijiji cha Namonge
Rwewenzewe mkoani Geita.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema hayo bungeni jana na
kuongeza kuwa watu hao waliuawa juzi alasiri.
Nyalandu alisema walishambuliwa kwa mawe walipokwenda kununua mahitaji
mengine na mafuta ya pikipiki wanayoitumia kwenye doria katika mapori ya
Hifadhi ya Moyowosi na Kigosi.
“Chanzo halisi cha mauaji hayo hakijajulikana, lakini tetesi zinasema hasira
za wananchi zilitokana na watu kukamatwa mara kwa mara kwa makosa ya ujangili
ndani ya mapori hayo ya akiba,” alisema.
Miili ya watu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Ushirombo wilayani
Bukombe.
Nyalandu alisema watu 15 walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo
kutokana doria iliyofanywa juzi na jana.
“Nilipigiwa simu na vijana waliokuwa wakifanya kazi na Kimaro huku wakilia,
inawapa hofu kuwa sasa wakivaa sare za uhifadhi wa wanyapori na kwenda
kijijini,” alisema Waziri Nyalandu.