Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro
Aliwataja waliofariki kuwa ni Joseph Peter (26) na Rajab
Nasoro (55) wote wakulima kutoka Kijiji cha Mbigili na mfugaji wa jamii ya
Kimasai, Kaduhu Kashu, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mabwegele. Wote walifariki
baada kuchomwa vitu vyenye ncha kali katika mapigano hayo.
Morogoro: Watu watatu wameuawa na wengine sita kujeruhiwa katika
mapigano yaliyozuka kati ya wakulima na wafugaji katika Bonde la Kilimo cha
Mpunga la Matembele, lililoko kati ya vijiji vya Mabwegere na Mbigili, Wilaya
ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Waliofariki; wawili wanatoka upande wa wakulima, ambao ni
wakazi wa Kijiji cha Mbigili na mmoja ni mfugaji kutoka jamii ya Kimasai
anayeishi katika Kijiji cha Mabwegere.
Kati ya waliojeruhiwa; wawili hali zao zinadaiwa kuwa ni
mbaya na hivyo, kulazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro
kwa matibabu zaidi.
Mapigano hayo
yalizuka juzi zikiwa zimepita wiki mbili baada ya nyumba 46 zilizokuwa
zikimilikiwa na baadhi ya wafugaji wa Kijiji cha Mabwegere na wakulima kuchomwa
moto na kundi linalodaiwa ni la wakulima, huku wafugaji wa jamii ya Kimasai
wakikimbia kuokoa maisha yao.
Akizungumza na
waandishi wa habari baada kuwatembelea majeruhi waliopo katika Hospitali ya
Misheni ya Mtakatifu Joseph, iliyopo katika mji mdogo wa Dumila, Mkuu wa Wilaya
ya Kilosa, Elias Tarimo, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo pamoja na
majeruhi.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Joseph Peter (26) na Rajab
Nasoro (55) wote wakulima kutoka Kijiji cha Mbigili na mfugaji wa jamii ya
Kimasai, Kaduhu Kashu, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mabwegele. Wote walifariki
baada kuchomwa vitu vyenye ncha kali katika mapigano hayo.
Waliojeruhiwa ni
Binzi Dotto (42) Shigele John, Juma Someke, Mohamed Athuman, Mbwana Athuman na
mfugaji, ambaye jina lake halijatambulika baada ya kukimbizwa na ndugu zake
katika hospitali isiyofahamika.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi, majira ya kati ya saa
9 na saa 10 jioni, baada ya wakulima
wanaokadiriwa kufikia 15 kutoka katika Kijiji cha Mbigili, kwenda katika
Bonde la Matembele wakiwa na matrekta kwa ajili ya kuanza kutayarisha mashamba
ya kilimo cha mpunga. Tarimo alisema siku mbili kabla ya tukio hilo, aliitisha
kikao cha maridhiano baina ya pande mbili hizo kwa ajili ya kupata suluhisho la
mgogoro wa bonde hilo, lakini upande wa viongozi wa kijiji cha wafugaji cha
Mabwegere haukufika katika mkutano huo.
Aliitupia lawama
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushindwa kupeleka
wasuluhishi wa mgogoro huo wa ardhi katika bonde hilo kama walivyoahidi.
Muuguzi wa zamu
katika hospitali hiyo, Milenia Shayo, alithibitisha kupokea miili ya watu
wawili na mmoja kufariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo,
alisema kupitia Afisa Habari wake, Nabwike Mwakatika, kuwa atatoa taarifa baada
ya kutoka kwenye eneo la tukio.