Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Shamariwa ‘A’, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Julias Makoye (CCM), amekutwa amejinyonga juu ya mti ulio jirani na nyumba yake usiku wa jana.

Makoye aliyetangazwa mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana, ameuongoza mtaa huo kwa awamu ya pili baada ya kuongoza miaka mitano iliyopita.

Akizungumza na NIPASHE jana nyumbani kwake, mke wa marehemu, Ivona Polikalapo, alisema saa 10 juzi jioni alimsikia mumewe akiongea na mtu kwenye simu yake ya mkononi na kumsisitiza anahitaji mzigo wake wote.

“Jana (juzi) saa 10 jioni nilimsikia mume wangu akiongea na mtu katika simu na kutaka alipwe mzigo wake wote kutokana na kukaa muda mrefu, lakini aliyekuwa akizungumza naye sikumfahamu ni nani,” alisema Polikalapo.

Aidha, alisema ilipofika saa 10 alfajiri ya jana, mbwa wao walisikika wakibweka kwa muda mrefu hali iliyomfanya marehemu atoke nje kuangalia kilichopo katika banda lao la mifugo huku (mke) akiendelea kuandaa chakula cha mifugo hao.

“Baada ya mume wangu kuamka na kwenda kuangalia kilichopo nje, hakuweza kurejea ndani hadi pale nilipotoka kwenda kumwaga uchafu shimoni nikashangaa baada ya kumuona ananing’inia juu ya mti…nilipojaribu kumuita hakuitika,” alisema.

Hata hivyo, mama huyo anasema haamini kama mume wake amejinyonga bali kanyongwa kutokana na mti aliojitundika kutoonekana kuwapo na jiwe la ‘sapoti’ ili kutekeleza azma yake hiyo.

Mashuhuda wa tukio hilo, Joseph Okala, alisema mwenyekiti huyo alikutwa akiwa amening’inia katika mti akiwa ameshakata roho.

“Baada ya kushuhudia hilo, watu walijaa eneo la tukio na kumuona mwenyekiti wao Makoye akiwa ananing’inia kwenye mti uliopo mbele ya nyumba yake lakini cha kushangaza haionyeshi kama alipanda juu kwani kamba ilikuwa imeshika sehemu za masikio na kidevu tu,” alisema Okala.

Hata hivyo, kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Japhet Lusingu, alithibitisha kuwapo na tukio hilo, akidai Makoye alijinyonga huku chanzo chake hakijafahamika.

“Ni kweli amejinyonga lakini sababu ya kufanya hivyo haifahamiki kabisa,” alisema Lusingu.
  CHANZO NIPASHE
 
Top