Watu watano wa familia moja waliouawa kinyama kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana wamezikwa kijijini kwao huku vilio vikitawala eneo la mazishi.
Tukio
hilo la kinyama lilijiri Septemba 28, mwaka huu saa 9:00 usiku katika Kitongoji
cha Kisesa Kata ya Bugalama Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wakati familia hiyo
ikiwa imelala ndani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Simiyu, Gemin Mushi alisema chanzo cha familia hiyo kuuawa kinyama kwa
kuchinjwa shingo ni mgogoro wa ardhi madai ambayo baadhi ya wanakijiji
wameyakanusha wakisema si sahihi sana.
Waliouawa katika tukio hilo ni George Charles (30), Siku John (23) mama wa
familia na watoto wao, Mchambi George (7) Tuma George (5) na Amos George (miezi
9). Wote walizikwa siku moja katika makaburi ya kijijini hapo.
Chanzo chetu kilifika katika
kitongoji hicho na kuzungumza na baadhi ya wanakijiji, majirani, ndugu na
wazazi wa marehemu na kubaini kuwa, chanzo kinachozungumwa au kuwemo akilini
mwa watu ni wivu wa maendeleo ya familia hiyo.
Baadhi ya wananchi ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini wakiwemo watu
wa karibu na familia hiyo, walisema chanzo ambacho kinaweza kusababisha tukio
hilo ni kujituma sana kwa marehemu George hivyo kuwazidi kiuchumi wananchi
wengine wa kijijini hapo.
Wananchi
hao waliyataja mambo saba ambayo wanaamini yalichangia wabaya wa George
kumvamia usiku na kumuua yeye na familia yake.“Kwanza kabisa marehemu alipoanza
kuishi eneo lile alilokutwa na mauti alikuwa kawaida. Halafu akaja akajenga
nyumba. Pili akafungua duka kubwa hapa kijijini.
“Tatu, marehemu alikuwa na
roho nzuri. Anakopesha kila mtu. Lakini nne ni jinsi duka lake lilivyokuwa
limejaza bidhaa nyingi kupita maduka mengine. Duka lake lilikuwa na kila
kitu.“Tano, nyumba ya marehemu George ndiyo iliyokuwa na umeme hapa kijijini
tena wa sola. Kwake mwanga usiku ulitofautisha nyumba yake na nyingine. Lakini
jambo la sita ni jinsi maisha yake na familia yalivyokuwa ya amani. Hilo nalo
naamini liliwaumiza wabaya wake.
“Saba, yule bwana mauzo ya
duka lake kwa siku yaliwazidi wafanyabiashara wengine wote. Kwa hiyo alikuwa
akikata mbuga kuelekea kweye mafanikio zaidi. Naamini wabaya wake
walipoyaangalia haya wakaona dawa yake ni kuimaliza hii familia,” alisema
mwanakijiji huyo.
Kauli hiyo ilionekana kuungwa
mkono na mjomba wa marehemu, Renatus Dutu kwa maelezo kuwa kutokana na
maendeleo yake marehemu, inawezekana baadhi ya wanakijiji walikuwa
hawayataki.“Nyumba yake ndiyo ilikuwa na umeme tu hapa kijijini. Alikuwa
akichaji simu nyingi za wananchi. Duka lake lilikuwa kubwa. Tuna wasiwasi
kwamba uwezo wake unaweza kuwa chanzo,” alisema Dutu.
Portini Shili ni jirani wa
familia iliyochinjwa ambapo anaeleza kuwa, chanzo hicho cha mgogoro wa ardhi
hakikubaliki na wanakijiji bali maendeleo ya familia hiyo kiuchumi ndiyo
yanasemwa kuchangia.
“Hilo eneo la ardhi
wanaloeleza polisi lilikuwa ni la mpwa wangu (mtoto wa dada yake). Wakati
wanauziana eneo hilo mimi nilikuwepo. Aliuziwa na baba wa kambo wa marehemu (George)
lakini wakati ananunua eneo hilo tayari familia ya George ilikuwa ikiishi humo
mpaka vifo,” alisema.
“Hakuna ukweli juu ya chanzo
hiki cha mgogoro wa ardhi na baba wa kambo ambaye anatuhumiwa na amekamatwa ni
mzee mwenye heshima hapa kijijini lakini hatuwezi kusema sana, sheria
inachunguza. Mimi nilikuwa ndani ya familia hiyo, mapenzi ya mzee huyo kwa
mtoto wake (George) yalikuwa makubwa sana kutokana na kuwasaidia,” alisema
Shili.
Mbali
na jirani huyo, baba mzazi wa mama wa familia, John Lutamba, ndugu wa marehemu
(Zengwe Sendama, mjomba (Renatus Dutu) nao walieleza kuwa hawaamini sana kama
chanzo cha vifo ni mgogoro wa ardhi kwa vile hakukuwa na mgogoro wowote katika
familia hizo.
“Hakuna ukweli wa juu ya
chanzo hicho mpaka sasa tupo tunajiuliza nini chanzo na wahusika ni akina nani?
Na hakuna mwenye jibu katika familia yetu, hakuna mgogoro wowote wa ardhi na
tulikuwa tunaishi vizuri,” alisema Lutamba.
Akizungumza na chanzo chetu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bugalama, Christopher Kulwa
alisema tangu amekuwa kiongozi katika eneo hilo hajawahi kusikia au kuletewa
ugomvi au mgogoro juu ya familia hiyo.
Alisema kama uongozi wa
serikali ya kijiji bado unafuatilia chanzo na wahusika wa tukio hilo ambapo
alisema katika hatua za awali za uchunguzi waliamua kila mwana kijiji kupiga
kura ya siri.
“Tumeendesha kura ya siri kwa
kila mtu ambaye anaweza kuwafahamu wahusika na chanzo. Kura hiyo tayari
tumepatiwa baadhi ya majina ya watu ambao walihisiwa kuhusika, tunayafanyia
kazi kwa kushirikiana na jeshi la polisi,” alisema mwenyekiti huyo.
Kamanda Mushi alisema kufuatia
mauaji hayo jeshi lake linawashikilia watu watatu ambao ni Migata Lusalago
(50), Jihelya Migata (30) na Sollo Kengele (31) wote wakazi wa kijiji hicho.