WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara nyingine ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ni watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote, waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia, alimpa meneja huyo wiki moja, kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).
Alitoa agizo hilo jana wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo, unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja, ikisema kontena limejaa diapers, lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner, ilionesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo, inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Kampuni ya Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo, kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo, ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao wa kazi, lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha Sh bilioni 13.5 ili waendeleze miundombinu ya reli, lakini hawakufanya hivyo.
“Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara, lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema. “Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa shilingi bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika, lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara.
Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu. Alipouliza wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza, wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari, wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.
 
Top