MKAZI wa kitongoji cha Kazima – Kichangani Kata ya Kawajense,
Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Emmanuel Joseph (31) amemfanyia unyama
mtoto wake wa kumzaa, George Emmanuel (4) kwa kuvichoma kwa moto vidole
vyake vya mkono wa kushoto, akimtuhumu kukomba mboga yote ya majani
aina ya ‘chainizi’ yenye thamani ya Sh 500.
Inasemekana baba huyo amekuwa akiishi na watoto wake watatu baada ya
kuachana na mkewe wa ndoa, Semsni Jahala (28) Machi mwaka jana.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Katavi, Rashid Mohamed akiwa mjini Mpanda alithitibisha kuwa
mkasa huo ulitokea juzi saa 12 jioni katika kitongoji cha Kazima–
Kichangani.
Akisimulia mkasa huo, Kaimu Kamanda Mohamed alisema mtuhumiwa huyo
amekamatwa kwa mahojiano na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada
ya upelelezi wa awali wa shauri lake kukamilika.
“Jioni hiyo ya tukio saa kumi na moja jioni mtuhumiwa huyo (Emmanuel)
alipika chakula cha jioni, ugali na mboga za majani maarufu chainizi
kisha akakihifadhi chakula hicho jikoni na kuondoka … aliporudi nyumbani
saa kumi na mbili jioni ili kuandaa chakula cha jioni ndipo alipobaini
mtoto wake (George) amekomba mboga yote ya majani. Alikasirishwa na
kitendo hicho na kusababisha kumpiga kisha kumchoma moto vidole vyake
vitatu vya mkono wa kushoto na kumsababishia maumivu makali,” alieleza
Kaimu Kamanda.
Kwa mujibu wa mashuhuda kutoka eneo hilo la tukio, mtoto huyo
alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako amelazwa kwa
matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Wilaya
ya Mpanda, Oscar Mkenda alisema mke aliamua kuachana na mumewe huyo
baada ya kuchoshwa na ukatili na unyanyasaji aliokuwa akifanyiwa,
ikiwemo kupigwa mara kwa mara bila ya sababu yoyote.
“Mtoto George alikomba mboga hizo zote za majani baada ya kushinda na
njaa mchana kutwa kwani hata kifungua kinywa hakupa asubuhi… hivyo
baada ya baba yake kubaini mtoto wake George amekomba mboga zote, ndipo
alipochochea moto na kuukandamiza mkono wake wa kushoto na kuunguza
vibaya vidole vyake vitatu,” alieleza Mkenda.
Muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Joseph Mkangwa alieleza
kuwa mtoto George amelazwa katika wadi namba nne kwa matibabu na kwamba
hali yake bado ni tete. Mtoto huyo anatunzwa hospitalini hapo na nyanya
yake, Hadija Ally