SERIKALI mkoani Kilimanjaro imeagiza kusimamishwa kazi mara moja
maofisa wanne kutoka Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya
Rombo kwa madai ya kuchochea kuwapo kwa migogoro ya ardhi, matumizi ya
vitabu bandia vya risiti na utendaji mbovu.
Kadhalika serikali imemtaka Katibu Tawala wa mkoa huo, Severine
Kahitwa, kuwarejesha wilayani hapa watumishi wawili wa idara hiyo ambao
wamehamishiwa katika wilaya za Siha na Mwanga ili kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla baada ya
kusikiliza kero na migogoro ya ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Holili
Wilaya ya Rombo ambako alijiridhisha kuwa maofisa hao wanahusika.
“Mkurugenzi fuata sheria zilizopo, hakikisha leo hii (jana) watumishi
hao wanaandikiwa barua za kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yao
na wewe Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) mnipe taarifa ndani ya siku 14 kuhusu
mazingira ya rushwa,” alisema Makalla.
Maofisa hao akiwamo Ofisa Ardhi wa Wilaya, Jovin Mtei na wengine
watatu kutoka Idara ya Upimaji wa Viwanja wamedaiwa kuwa tatizo huku pia
wakidaiwa kuuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili.
Mkuu wa mkoa aliwataja maofisa wengine wanaotakiwa kusimamishwa kuwa
ni Mkuu wa Idara, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Arbogast Mhumba;
Mpimaji Ardhi Msaidizi, Mipawa Richard na mwingine Bartholomew Urassa.
Makalla pia aliwataja watumishi ambao Katibu Tawala Mkoa anatakiwa
awarejeshe wilayani hapa kuwa ni Ofisa Mipango Miji Wilaya ya Siha, John
Mpanju na Mpimaji wa Ardhi Msaidizi Wilaya ya Mwanga, Ulomi A ambao kwa
nyakati tofauti walifanya makosa mbalimbali wakiwa watumishi wa Wilaya
ya Rombo.