MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete
amesema hajahusika kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar kwa kumpigia simu
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Aliyasema hayo juzi mjini hapa wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi
ya Chama ya Kibaha Mjini mkoani Pwani na kusema maneno hayo ni ya uongo,
hayana ukweli wowote na watu hawapaswi kutoa shutuma hizo juu yake.
Rais huyo wa Awamu ya Nne alisema maneno hayo hayana kichwa wala
miguu wala hajawahi kumpigia simu Jecha kwa ajili ya kuzungumzia masuala
ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwani tume hiyo inajitegemea.
“Wasitoe lawama zisizohusika, wapuuzeni sikuwahi kufanya hivyo hata
kwa Damian Lubuva wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania hivyo
nashangaa watu wanavyosema kuwa nimehusika kufutwa uchaguzi huo,”
alisema Kikwete.
“Tume ya Zanzibar ni tume huru na inajitegemea kwani ina mambo yake
hata Dk Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) hana uwezo wa kuingilia na
kuahirisha uchaguzi huo, watu hao wasipake watu matope wasio husika
kwani kila mtu ana nafasi yake,” alifafanua Kikwete.
Alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuwaombea Wazanzibari wafanye
uchaguzi wao mkuu wa marudio kwa amani na utulivu ili wapate viongozi
wao wa kuiongoza Zanzibar na wawaombee wagombea wa CCM washinde.
Aidha, alisema chama hicho kinapaswa kuwaadhibu watu waliokihujumu
chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutomwonea mwanachama,
bali watende haki na si kwa kwa uonevu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao
alisema Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameonesha njia ya
kiongozi kutumia fursa kuboresha mazingira ya utendaji kazi Awali, Koka
ambaye ndiye aliyejenga ofisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 100,
alisema aliamua kujitolea kujenga ofisi hiyo kwa lengo la kukisaidia
chama kiendeshe shughuli zake.
Koka alisema aliamua kujenga kama kumbukumbu kwa wanaKibaha ili iwe
kielelezo cha uongozi wake kama mbunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya
kufanya shughuli za chama badala ya kufanyia sehemu zisizo na hadhi yao.