Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Olouch, amesema
matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni ni batili kwa
kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako, hakuzingatia sheria kufuta mfumo wa wastani wa alama (GPA)
kwenda madaraja (division).
Kadhalika, amesema waziri alitakiwa kufanya mabadiliko ya kanuni na
kuzitangaza katika Gazeti la Serikali (GN) na bila kufanya hivyo upo
uwezekano wa wanafunzi kuishtaki.
Akitoa maoni yake binafsi kwa Nipashe jana kwa njia ya simu,
alisema Sheria ya Baraza la Mitihani kifungu cha 18 kinampa nguvu waziri
kutunga kanuni za kupanga matokeo (grading system), lakini waziri huyo
kabla ya kutoa tangazo katika GN aliutangazia umma kubadili mfumo wa
upangaji matokeo hayo.
Alisema Novemba 25, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alitoa kwenye gazeti la
serikali tangazo la kubadili kanuni za upangaji matokeo kutoka kwenye
madaraja kwenda GPA, na kwamba Waziri Ndalichako ameendelea kutumia
kanuni hizo na kubadili mfumo.
“Kwa hali ilivyo ni wazi kuwa kanuni za kukokotoa matokeo
inayoendelea kutumika ni zilizowekwa na waziri wa serikali ya awamu ya
nne, hatujaona GN ya Serikali kuhusiana na mabadiliko haya ya sasa, hili
limeleta mgogoro mkubwa katika elimu na serikali isipokuwa makini
itasababisha wanafunzi kwenda mahakamani,” alisema.
Alisema alichotakiwa kukifanya Prof. Ndalichako, ni kutengua kanuni
za awali na kuziweka katika GN ili liwe suala rasmi, lakini hakufanya
hivyo.
“Kutokana na waziri kutotengua kanuni na kutangazwa katika Gazeti
la Serikali, naye hajatunga kanuni kwenye mchakato wa sheria, hivyo
matokeo ya kidato cha nne ni batili," alisema.
Kadhalika, alisema kama hatua ya kuwataka waliopewa matokeo ya GPA
warudishe vyeti ni ili kutaka wabadilishiwe kwenda kwenye madaraja, ni
kinyume cha sheria, huku akifafanua kuwa hajawahi kuona sheria inafanya
kazi kwa kurudi nyuma.
Oluoch alisema ili matokeo ya sasa yawe halali ni lazima waziri
aheshimu na kufuata sheria na kanuni hata kama kuna sheria namba 20 ya
Necta inamruhusu kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na baraza hilo, ili
kuepuka mkanganyiko na siasa kupenyezwa katika elimu.
“Kifungu cha 20 cha sheria ya Baraza la Mitihani ya mwaka 1973 na
marekebisho yake, kinasema waziri anaweza kutoa maelekezo ila siyo
yanayokizana na kanuni ambazo zipo, alichokifanya waziri ni kukizana na
kanuni zilizopo kwa maelekezo yake kwa Necta,” alisema na kuongeza:
“Utungaji wa sheria huwezi ukarudi nyuma, huwezi kusema waliopewa
GPA wapewe kwa madaraja, itakubalika kwa sheria ikiwa matokeo kuanzisha
madaraja yatafaidisha waliokwisha fahidika na GPA na kuwa na sifa za
kwenda vyuo vikuu, vinginevyo mwanafunzi akienda kulalamika mahakamani
atasikilizwa kwa kuwa kuna ukiukwaji wa sheria,” alisema.
Aidha, alimshauri waziri kuomba ushauri wa kisheria juu ya mkanganyiko huo ili asiitumbukize nchi kwenye mgogoro wa matokeo.
Pia, alisema utaratibu wa kurudisha vyeti utaathiri vyuo vingi
ambavyo vilishawapokea wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya vizuri
chini ya mfumo wa GPA ambao uliwapendelea waliofanya vibaya.
Msemaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Olver
Kato, alipoulizwa kama waziri alitoa kwenye Gazeti la Serikali tangazo
la mabadiliko ya kanuni, alisema waziri anaishia kutamka na Necta ndiyo
wanajua walitumia utaratibu gani kutangaza matokeo, hivyo waulizwe juu
ya suala hilo.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk. Charles Msonde, simu yake haikupokelewa na alivyotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.
Chanzo: Nipashe