Serikali imetoa tahadhari ya mlipuko wa kimeta, moja ya magonjwa
yanayoenezwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, katika mkoa wa
Kilimanjaro.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Wizara ilisema siku za karibuni ugonjwa wa Kimeta ulitokea mkoani
Kilimanjaro ambapo wagonjwa 23 waliugua na kuripotiwa katika kijiji cha
Rauya, kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini.
Taarifa ilisema ugonjwa huo ulianza kwa mgonjwa mmoja aliyeugua
baada ya kuchinja ng'ombe na mbuzi waliokuwa wamekufa ambaye; alitibiwa
katika hospitali ya KCMC na kupona.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na
Wizara ya Kilimo pamoja na timu ya Mkoa na Wilaya ilifanya uchunguzi.
Katika uchunguzi huo, imeelezwa, ilibainika kuwa watu 23 waliugua
na walihusika moja kwa moja katika uchinjaji au upishi wa nyama za
ng'ombe wagonjwa au waliokufa waligundulika kuwa na dalili za ugonjwa wa
Kimeta.
Taarifa ilisema timu ya wataalamu wa afya kutoka ngazi ya Taifa
ilikwenda kushirikiana na timu ya Mkoa na Wilaya husika katika uchunguzi
na udhibiti wa ugonjwa.
“Ufuatiliaji wa waliokula nyama ya ng'ombe waliougua au kufa
ulifanyika ambapo wote wamepata dawa za kinga, jumla ya watu 904
walihusishwa na kula nyama za ng'ombe waliokwishakufa ambapo Wilaya ya
Siha ni 836 na Wilaya ya Moshi Vijijini walikuwa 68,” ilisema taarifa ya
Wizara.
"Ugonjwa wa Kimeta unasababishwa na aina ya bakteria aitwaye
Bacillus anthracis ambaye anashambulia wanyama mwitu, wafugwao pamoja na
binadamu."
Taarifa ilifafanuwa kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kutoka mnyama
kwenda kwa binadamu au kutoka binadamu mmoja kwenda mwingine au kwa njia
ya kugusa nyama, damu na majimaji kutoka kwa mnyama au mwilini mwa mtu
aliyeambukizwa ugonjwa huo kutokana na kula nyama ya mnyama aliye
mgonjwa.
“Wizara inatoa rai kwa jamii kuchukua tahadhari za kujikinga na
ugonjwa huu ambazo ni pamoja na kuepuka kula nyama inayotokana na mnyama
aliye mgonjwa au aliyekufa," ilisema taarifa hiyo na kusisitiza
wananchi wanapaswa kutumia nyama iliyothibitishwa na mtaalamu wa
mifugo.”
Chanzo: Nipashe