Rais Dk. John Magufuli, amemrudisha nyumbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, pamoja na watumishi wengine watano, baada ya muda wao kumalizika.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Dk. Magufuli kuwarejesha nyumbani Mabalozi wa Tanzania walioko nchi za nje baada ya muda wao wa mkataba kumalizika.
Ikumbukwe kuwa Januari 25, mwaka huu, Rais Magufuli alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, kuja kufanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk. James Msekela na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk. Batilda Buriani, baada ya mikataba yao kumalizika.
Akizungumza na Nipashe, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, alisema kurudhishwa nyumbani kwa Balozi Msuya, ni jambo la kawaida kwa sababu bado kazi ya kuwarudisha nyumbani Mabalozi waliomaliza mikataba yao linaendelea.
Alisema kwa sasa serikali inachofanya ni kuwarudisha nyumbani Mabalozi ambao mikataba yao imemalizika na kuwapeleka watumishi wengine wakapate uzoefu nje ya nchi.
Alisema kuna makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni watumishi wa idara ambao muda wao wa miaka mitano umemalizika ambao wanarudishwa nyumbani ama kuhamishiwa kituo kingine cha kazi.
Alisema kundi la pili ni la Mabalozi ambao siyo watumishi wa wizara, lakini waliteuliwa na Rais kwa mkataba, hivyo mikataba yao ikimalizika Rais mwenyewe ndiye anayeamua kama ni kuwaongezea au kusitisha na kurudi nyumbani.
Dk. Mahiga alitaja kundi la tatu kuwa ni Mabalozi ambao muda wao wa kukaa nje umemalizika au umri wao wa kustaafu umefika, lakini mikataba yao bado haijamalizika, hivyo Rais anaamua kuwarudisha nchini ili wapumzike na wengine wakashike nafasi zao.
Alisema kuna Mabalozi ambao mikataba yao ya kufanya kazi nje ya nchi ni miaka mitano, lakini wamekaa zaidi ya miaka 10, hivyo serikali iko katika mchakato wa kuwarudisha nyumbani.
Waziri Mahiga alisema kuna vituo zaidi ya 35 ambavyo vinatakiwa kuwa na Mabalozi, hivyo serikali itahakikisha inawarudisha nyumbani mabalozi waliomaliza muda wao wa kazi na kupangiwa majukumu mengine.
Chanzo: Nipashe