MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala amewaokoa mkuu wa wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Jamuhuri Wiliam kutoathiriwa na hasira za wananchi waliokuwa wakishinikiza serikali kuweka matuta katika barabara kuu ya Dar kwenda Moshi, eneo la Kileo wilayani Mwanga kwa madai ya kuchoshwa na ajali za mara kwa mara.
Zaidi ya wananchi 500 waliifunga barabara hiyo kwa mawe, magogo ya miti wakizuia magari zaidi ya 300 kuendelea na safari zao wakitokea wilaya za Moshi, Rombo, Siha na Hai kwenda nje ya mkoa wa Kilimanjaro na yale ya nje ya mkoa kutoingia mkoani hapa.
Makalla, ambaye alikuwa ameitisha kikao cha kazi na wakuu wa wilaya zote za mkoa, wakurugenzi, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na watendaji wengine wa serikali, alikieleza kikao hicho kwamba mkuu wa wilaya ya Mwanga na mkurugenzi wake hawatahudhuria.
”Nimepokea udhuru wa mkuu wa wilaya ya Mwanga na mkurugenzi wake, wamezuiwa na wananchi eneo la Kileo, ikiwa ni baada ya mwendesha pikipiki kugongwa na gari na kufa...wananchi wanadai wamechoshwa na ajali, wanataka matuta au alama za barabarani eneo hilo,” alisema.
Makalla alisema kulingana na mazingira hayo ilimlazimu kupiga simu na kumtaka mkuu wa wilaya kuweka sauti ya juu ili awatulize wananchi waliohitaji kauli ya serikali mkoani humo kuhusu kuwekwa kwa matuta au alama zinazoashiria kupunguzwa mwendo kwa magari katika eneo hilo.
”Baada ya kauli yangu angalau wananchi walielewa na kuondoa vizuizi vilivyokuwa barabarani na hivyo magari kuendelea na safari lakini hiyo isingewezesha mkuu wa wilaya pamoja na mkurugenzi kuwahi kikao,” alisema.
Kutokana na kadhia hiyo, mkuu wa mkoa alimuagiza meneja wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Kilimanjaro, Mwita Rubirya, kuhakikisha wanaweka matuta katika eneo hilo linalolalamikiwa na wananchi