Dilukwili alisema maeneo mengi ya vijijini yamekuwa na
sifa zinazoogopesha wageni wanaofika katika maeneo yao kwa kuendekeza
ushirikina.
Mvomero. Imeelezwa kuwa imani za kishirikina ndiyo chanzo
cha walimu kushindwa kufundisha maeneo ya vijijini pindi wanapopangiwa kutokana
na kutishiwa maisha wanapotoa adhabu kwa wanafunzi wao.
Mratibu Elimu Kata ya Mvomero, Malonga Dilukwili alisema
hayo jana alipozungumza na walimu, maofisa watendaji wa vijiji na madiwani
kwenye mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika elimu yaliyoandaliwa
na Asasi ya Elimu na Mazingira (Wetu) mkoani hapa.
Dilukwili alisema maeneo mengi ya vijijini yamekuwa na
sifa zinazoogopesha wageni wanaofika katika maeneo yao kwa kuendekeza
ushirikina.
“Inasikitisha, walimu wamekuwa wakijitolea kufundisha
lakini wenyeji wanawatolea maneno ya vitisho kuwa wataondoka. Sasa kwa mtindo
huu elimu itapanda maeneo ya vijijini?” alihoji Dilukwili.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk Joseph Saqware alisema ili
elimu ikue maeneo ya vijijini, ni lazima wazazi na walimu washirikiane katika
kukuza sekta hiyo. Alisema licha ya walimu kuogopa, lakini miundombinu ya shule
za vijijini haikidhi vigezo vya kufundishia wanafunzi.
Aliiomba Serikali kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya
shule hizo, huku akisisitiza wazazi na walezi kuacha kuwatolea walimu lugha za
kutisha.
Chanzo: Mwananchi