Ni kuhusiana na mikataba
mbalimbali aliyoingia.
Mwanza. Chadema kimesema kinaishanga Serikali kumtoa sadaka
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka na kumuacha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
akiendelea kutumia fedha za umma kwa kuzunguka mikoani.
Pia, chama hicho kimehoji kuwa Profesa Tibaijuka na mikataba ya nishati ni
wapi na wapi na kwamba kumuacha Profesa Muhongo bila kumuwajibisha ni kuendelea
kuifanya Serikali izidi kuchukiwa na wananchi bila sababu ya msingi.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara juzi uliyofanyika kwenye Viwanja vya
Furahisha na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mkoa huu, naibu Katibu mkuu wa
chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Serikali kuendelea kumuacha Waziri
wa Nishati na Madini ni jambo la ajabu, kwani yeye ndiye mtu aliyepaswa
kuwajibishwa awali.
“Unajua kitu tunachokiona hapa ni jambo la kushangaza. Mhusika mkuu wa mambo
yote yanayohusu mikataba ya nishati anaachwa halafu mtu anayeshughulikia
masuala ya ardhi anakuwa mtu wa kwanza kuwajibishwa kama siyo kumtoa sadaka ni
nini,” alihoji Mwalimu.
“Leo Profesa Muhongo anaendelea kutumia fedha za umma kwa kuzunguka mikoani
na kutoa ahadi ambazo hawezi kuzitekeleza. Chadema hatutakubali kuona CCM
inaendelea kuwanyonya wananchi, lazima mabadiliko ya kweli ya fanyike mwaka
huu,” alisema.
Naibu katibu mkuu huyo wa Chadema Zanzibar alisema wamekuwa wakiona na
kusikia kwamba kuna viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakija Mwanza kwa madai ya
kuweka mikakati ya kukomboa majimbo yanayoongozwa na Chadema, lakini watambue
majimbo hayo hayatarudi kwao.
Mwalimu alisema kila mbinu zinazofanywa na CCM kipindi hiki wanazitambua na
kwamba chama chao kipo imara kila idara, kwani picha nzuri tayari wameionyesha
kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Tunajua kuna vigogo wa CCM wamekuwa wakija Mwanza, kwa madai ya kutaka kuja
kukomboa majimbo yaliyochukuliwa na Chadema, lakini tambue wao wakiwaza kufanya
hivyo sisi tumeshawaza mbele zaidi na picha wameiona kwenye uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.”
Aidha, Mwalimu alipinga hatua ya Tume ya Uchaguzi kuruhusu jeshi kusimamia
Uchaguzi Mkuu mwaka huu, huku akieleza kuwa kazi ya jeshi ni kulinda mipaka
siyo uchaguzi.
Mwalimu jana aliwatembelea wafuasi wa chama hicho waliopo kwenye Gereza la
Magu, ambao waliokamatwa kwa madai ya kufanya vurugu.
Crdt: Mwananchi