
Anaongeza: “Wengi wanatumia njia za mkato kujipatia mali kwa kuondoa uhai wa wengine. Ukichunguza kwa umakini utagundua kwamba mipango ya mauaji inafanywa na wanafamilia.’’
Mwenyekiti wa chama cha watu wanaoishi na Ukimwi Wilaya ya Bukombe, Essau
Malifedha anasema katika mila za Kisukuma, kuna mambo kadhaa kama vile
kuchelewa kwa mvua. Anasema zinapochelewa jamii humhisi kikongwe yeyote kuwa
ndiye aliyesababisha hali hiyo.
“Usukumani mvua zinapochelewa kunyesha, wanaamini kwamba ni mwanamke mzee na
moja kwa moja wanakimbilia kupiga ramli. Wakati mwingine ni tamaa za mali,
unakuta mzazi anamrithisha mali mtoto akiwa mdogo, sasa wanapokua wanaona mzee
hafi wanaamua kumuua ili warithi,” anasema Malifedha na kuongeza kuwa mtazamo
huo ni athari itokanayo na ujinga.
Anaongeza kuwa mauaji kwa wazee yanatofautiana kutoka eneo moja hadi
jingine… “Ukiona shingo imekatwa mara moja unajua ni kabila gani limehusika na
mauaji, kama panga limekata zaidi ya mara mbili ni kabila jingine vivyo hivyo
na maeneo ya mwili na marehemu.”
Kubini Nkondo kutoka shirika la Nabroho Society For The Age liliyopo Simiyu
anasema uchawi una uhusiano na mauaji ya wazee wengi.
“Tunachokiona hapa mauaji ya wazee hayana uhusiano na uchawi japokuwa
wanaoua huweka dhamira hiyo, kwa kwani takwimu hazipungui na kama ni kweli
tungeona wamepungua.
“Kwa mfano, mwaka 2008 huko Magu- Chandulu kuna mzee mmoja alikatwa mapanga,
siku moja baadaye kuna watu walisikika wakidaiana ujira klabuni,” anasema na
kuongeza:
“Lakini kumbe walidhulumiana na hapo ndipo kijiji kilipojua kumbe waliua kwa
ajili ya mali na si uchawi waliomtuhumu. Mwaka 2007, kuna mzee aliuawa kwa
ajili ya kusuluhisha ugomvi wa wanandoa, huko kwetu hakuna usawa kijinsia,”
anasema Nkondo.
Sera ya Taifa ya Wazee
Bifandimu anahoji kwa nini imani hizi zinasababisha mauaji mengi ya wazee na
bado hakuna mikakati mahususi ya kuwanusuru?
“Sera ya Taifa ya Wazee (Nap) ndiyo pekee inayolaumu mila potofu ikiwa ni
pamoja na mauaji ya wazee kwa tuhuma za uchawi, lakini kwa bahati mbaya, sera
hii bado haijatungiwa sheria. Mkukuta inayoelekeza jinsi masuala ya wazee
yatakavyoshughulikiwa bado haijalishughulikia suala la mauaji ya wazee,”
anasema.
Anasema Tanzania inazo sheria mbalimbali ambazo zinalenga kuwalinda wazee
kama raia wengine, lakini kesi nyingi zinazohusiana na mauaji ya wazee zimekuwa
zikiishia njiani kwa maelezo kuwa hakuna ushahidi wa kutosha na hivyo kuendelea
kuuawa kwa tuhuma za uchawi.
Chanzo Mwananchi