SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema mazungumzo yanayoshirikisha viongozi wa vyama viwili vya siasa vya CCM na CUF, yanaendelea na hakuna makubaliano yaliyofikiwa hadi sasa ya kurudiwa kwa uchaguzi mkuu uliofutwa wa Oktoba 25.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya taarifa za vyombo vya habari zilizotolewa ambazo zimepotosha ukweli wa mazungumzo hayo.
Akifafanua zaidi Balozi Seif alisema mazungumzo yanayoshirikisha viongozi wa pande mbili za vyama vya siasa vya CCM na CUF yanaendelea hadi sasa na taarifa kamili ya makubaliano yaliyofikiwa itatolewa kwa wananchi.
Alisema hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya pande mbili hizo kuhusu suala la kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), baada ya kujitokeza kwa kasoro mbali mbali za ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
“Napenda kuwajulisha wananchi kwamba mazungumzo ya pande mbili za vyama vya siasa CCM na CUF yanaendelea vizuri na taarifa zaidi wananchi watajulishwa, lakini hadi sasa hakuna tulichokubaliana ikiwemo suala zima la kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Balozi alivionya vyombo vya habari kuwa makini katika utoaji wa taarifa wa suala hilo, ili kuepuka upotoshaji unaoweza kusababisha malumbano na kuchafuka kwa hali ya hewa. Hivi karibuni Balozi Seif alifanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Ufaransa (RFI), ambapo alisema mazungumzo yanayohusisha viongozi wa vyama vya siasa vya CCM na CUF, hayajafikia makubaliano ya kurudiwa kwa uchaguzi.
“Nilichosema mimi ni kwamba mazungumzo yanayoendelea ya vyama vya siasa hayajafikia makubaliano, ikiwemo suala la kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu... lakini nilisema kwamba Chama Cha Mapinduzi kipo tayari kurudia uchaguzi kama itakubaliwa kufanya hivyo,” alisema.
Vyama vikuu vya CCM na CUF vimekuwa na msimamo tofauti katika suala la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba uliofutwa na ZEC ambapo msimamo wa CCM na kurudiwa kwa uchaguzi huo kutokana na kasoro zake.
Hata hivyo hadi sasa CUF, imesisitiza kwamba haipo tayari kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa mujibu wa taarifa za Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.
Chanzo: HabariLeo
 
Top