NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni
ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasimamisha kazi askari watatu wa Kikosi
cha Zimamoto cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),
Dar es Salaam kutokana na tuhuma za wizi wa mafuta ya ndege pamoja na
mizigo ya abiria.
Alitaja majina ya askari hao kuwa ni Abias Mwanza, Khalfani Kisana na
Musa Mandauli ambao wote wanatoka Kikosi cha Zimamoto katika JNIA.
Aidha, Naibu Waziri ameiagiza Idara ya Uhamiaji kwenye uwanja huo wa
ndege kufanya uhakiki wa mapato yanayotokana na viza zinazotolewa kwa
wageni kwani imebainika kuwa idadi ya viza zinazotolewa kwa wageni
hailingani na mapato yanayopatikana.
Masauni alitoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam jana, alipofanya
ziara kwenye vitengo mbalimbali vya kiwanja hicho, ikiwa ni sehemu ya
ukaguzi wa taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, ikiwamo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji.
Katika ziara hiyo ambayo ilianzia Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na
kwenda JNIA kisha Kituo cha Polisi cha Buguruni katika Wilaya ya Ilala,
Naibu Waziri Masauni alikiri kwamba licha ya kazi nzuri inayofanywa na
Jeshi la Polisi, lakini bado uaminifu kazini bado ni changamoto kwa
baadhi ya askari.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Agosti 26, mwaka jana askari Kisana na
Mandauli wanatuhumiwa kukamatwa na dumu 10 za ujazo wa lita 20 zikiwa
zimejaa mafuta ya ndege zikisafirishwa kutoka kiwanjani hapo kwa kutumia
gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili STJ 2948 ambalo ni la
Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto JNIA.
Mtuhumiwa Mwanza ambaye pia ni askari anatuhumiwa kushirikiana na
mfanyakazi wa Kampuni ya Swissport, Lucas Maganda baada ya kunaswa na
kamera za kiwanjani hapo wakishirikiana kutoa mizigo ya abiria kinyume
cha utaratibu kutoka kwenye eneo la kuhifadhia mizigo.
“Naagiza askari hawa wasimamishwe kazi mara moja ili kupisha
uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili,” alisema Naibu Waziri na
kuongeza kuwa wakibaini kama makosa wachukuliwe hatua kali za kisheria.