Ikiwa ni siku tatu tangu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mawasiliano
ya Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad, atangaze kuwa
baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanakimbilia porini kuhofia usalama wao,
ametiwa mbaroni.
Kukamatwa kwa Masoud sasa kunafanya idadi ya viongozi wa chama
hicho waliotiwa mbaroni na kuhojiwa polisi kufikia wanne tangu kufutwa
kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka jana.
Viongozi wengine waliohojiwa na Polisi na kuachiwa kwa dhamana ni
Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui, Mkurugenzi wa Mipango na
Uchaguzi, Omar Alin Shehe na mshauri wa mikakati wa chama hicho, Eddy
Riyami.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis
Mkadam, jana alithibitisha kukamatwa kwa Masoud, ambaye ni Waziri wa
zamani wa Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Umoja wa
Kitaifa.
Alisema kiongozi huyo alikamatwa na kitengo cha upelelezi nyumbani kwake mtaa wa Mbweni mjini Zanzibar jana.
Alisema kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe
Madema ili kusadia uchunguzi juu ya taarifa alizotoa katika mkutano wake
na waandishi wa habari na kuzungumzia hali ya amani ya Zanzibar na
wananchi wake.
“Tunamshikilia kwa uchunguzi, kuna mambo ya msingi tunaona
yanahitaji kufanyiwa uchunguzi na yeye kusadia polisi uchunguzi wake,”
alisema Mkadam.
Kufuatia kukamatwa huko kwa Masoud, CUF imelaani kitendo hicho na
kusema kuwa kamata kamata hiyo inawalenga viongozi wa chama hicho na
wanachama wake pekee.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mazrui alisema matukio yote ya
uvunjifu wa amani yaliyotokea visiwani hapa, yamekuwa yakihusishwa na
CUF na Jeshi la Polisi huwakamata viongozi wa chama hicho pekee.
“Tunasema huu ni uonevu wa hali ya juu, maana viongozi na wafuasi
wa CUF pekee ndio wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi, hii yote inatokana
na uchaguzi wa marudio, hivyo kutoshiriki kwetu kwa uchaguzi isiwe
sababu ya kuadhibiwa,” alisema.
Aidha, alisema suala la kushiriki au kutoshiriki katika uchaguzi ni
hiari ya mtu, hivyo kwa wale ambao hawatashiriki uchaguzi huo,
wasiadhibiwe wala wasidhalilishwe na wale ambao wametangaza kushiriki
waende wakapige kura.
Kamishna wa Jeshi hilo, Hamdani Omar Makame na Kamanda Mkadam kwa
nyakati tofauti, walisema watu 42 wanashiliwa na jeshi hilo kutokana na
matukio ya uvunjifu wa amani yaliotokea Unguja na 31 kuhusiana na
matukuo yaliotokea Pemba.
Aidha, walisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuwajua
wahusika wa matukio hayo ili kuwafikisha mahakamani, lakini pia
linafanya uchunguzi ili kufahamu ni aina gani ya bomu lilitumika katika
ulipuaji wa nyumba ya Kamishna wa Polisi iliyopo Kijichi nje ya mji wa
Zanzibar.
Kwa upande wa mke wa Masoud, Rahma Issa, alisema askari kazu
wasiopungua sita wakiwa na silaha za moto mbili walifika nyumbani jana
saa moja asubuhi na kudai wanamhitaji mumewe.
Alisema baada ya kubisha hodi, kijana wake mmoja alifungua mlango
na kisha askari watatu waliingia ndani mmoja akiwa na silaha ya moto
kifuani.
“Baada ya kuamshwa na kutoka chumbani walimwambia yupo chini ya ulinzi anahitaji kituo cha polisi,” alisema Rahma.
Hata hivyo, alisema baada ya kumkamata, hawakumwambia sababu ya
kukamatwa kwake, lakini baada ya kuwauliza wanampekeka kituo gani
walimwabia Kituo cha Polisi Mwembe Madema, Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe,
alisema vitendo vya kukamatwa viongozi wa CUF ni mwendeleo wa Serikali
ya CCM kuwanyanyasa viongozi na wanachama wake chama hivyo visiwani
hapa.
Alisema vitendo vnavyoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi vinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia na haki za binadamu.
Shehe alisema matunda ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kujenga
amani na umoja wa kitaifa yameanza kuvurugwa tangu kuingia mgogoro wa
uchaguzi mkuu.