Rais John Magufuli, ameponda Mkataba wa Serikali na Kampuni ya kufua
umeme ya IPTL, akisema wakati umefika nchi iachane na umeme wa
wafanyabiashara na iwe na wake yenyewe.
Akiweka jiwe la msingi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi
II, Rais Magufuli alisema: “Ni lazima nchi yetu tuachane na umeme usio
na uhakika, umeme wa kukodishakodisha, umeme wa kutumia watu na ndiyo
maana kumekuwa na matatizo mengi mara IPTL, mara nini, ni kwa sababu
tulizoea maumeme ya kukodisha kodisha, ya wafanyabiashara, kwa hiyo
hatua hii ya umeme wetu, ambao tutaumiliki sisi wenyewe tutafanikiwa
katika maendeleo.
“Tuachane na mitambo ya kukodi, tumechoka kufanyishwa biashara na
wawekezaji, tunalipia `capacity charge' za ajabu ajabu halafu tunalipia
bei ya ajabu.
“Tunawapa shida Watanzania wa hali ya chini, kila mmoja anahitaji
umeme, lakini wengine wanashindwa kuuvuta kwa sababu umeme ni wa juu.”
Katika kashfa ya Tegeta Escrow iliyosababisha kutafunwa kwa
takribani Sh. bilioni 300, mbali na kung’oa baadhi ya mawaziri na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baadhi ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge
mpaka leo hakuna kilichofanyika.
Azimio la saba la Bunge lilisema kwa kuwa taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuwa, Tanesco
imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa
na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya shirika hilo, serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa shirika la umeme nchini kwa lengo la kuokoa fedha.
Agizo hilo lililotolewa mwishoni mwa mwaka 2014, lakini mpaka leo
halijatekelezwa na inadaiwa kuwa kila mwezi Tanesco inailipa IPTL Sh.
bilioni nane, izalishe ama isizalishe umeme.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
iliyowasilisha ripoti yake Bunge la 10 juu ya Escrow, alisema: “Mapato
ya nchi makubwa kuliko ya utumbuaji majipu yanaendelea kupotea. Mkataba
wa IPTL bado unaendelea kunyonya nchi na serikali inatazama Sh. bilioni
nane zinalipwa IPTL na PAP kila mwezi. Katika siku 100 tangu Rais
Magufuli aingie madarakani, jumla ya Sh. bilioni 30 zimeshalipwa kwa
IPTL/PAP.”
UMEME MUHIMU
Rais Magufuli alisema umeme ni kichocheo muhimu katika ukuaji wa
uchumi popote duniani na kwamba matumizi ya nishati hutumika kama kipimo
cha maendeleo ya nchi husika.
“Hutumika kuongeza ufanisi katika shughuli za uchumi na kuboresha
huduma za kijamii kama elimu afya.. bila ya umeme wa uhakika ndoto ya
uchumi wa viwanda haitatimia, tutakapokuwa na umeme maana yake ndoto ya
kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa itafanikiwa na vitatengeneza
ajira,” alisema.
Rais alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, uwezo wa nchi wa kuzalisha umeme ni takriban megawati 1,200 kwa mwaka.
“Taarifa za waziri leo tumefikia megawati 1,026, hivyo kila
Mtanzania anatumia voti 30 kwa mwaka, ikilinganishwa na nchi
zilizotuzunguka mfano Kenya kila Mkenya anatumia voti 40 kwa mwaka,
China voti 490 kwa mwaka, Afrika Kusini voti 500 kwa mwaka, Marekani
kila Mmarekani anatumia voti 1,683 kwa mwaka, kwa hiyo sisi bado tupo
chini,” alisema.
Rais Magufuli alisema kwa kutambua hilo, wakati wa kampeni za
uchaguzi zilizofanyika mwaka jana walizungumzia kuhusu adhma ya nchi
iwe ya viwanda, lakini walitambua hawawezi kufanya hivyo bila kuimarisha
umeme.
“Leo nimefarijika kuona katika kipindi cha miezi mitatu na ushee
nikiwa madarakani nimealikwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi
II utakaotoa megawat 240, hii ni hatua nzuri.
“Ninafahamu mradi huu ulikwama siku nyingi, serikali ya Japan
iliamua kutupa Dola zinazokadiriwa kufika milioni 300, lakini sharti lao
kubwa tuchangia asilimia 15 (Dola milioni 120) na Japan Dola milioni
292 . Tumekaa zaidi ya miaka miwili tukiwa tumeshindwa kuzipata asilimia
ya dola hizi ili tupate zao,” alisema.
Aliongeza kuwa aada ya kuimarika kwa makusanyo Novemba na Desemba,
mwaka jana, walitoa maelekezo zikapatikana fedha hizo, ndipo wajapani
nao walipotoa Dola 292.
TANESCO NA WIZARA
Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba yeye ni mgumu kupongeza, lakini kwa jitihada zilizofanyika wamekwenda kwenye mwelekeo.
“Tanzania ni tajiri, tuna gesi ya kutosha kwa taarifa zilizopo tuna
futi za ujazo zaidi ya trilioni 57, kwa hiyo kila mahali kuna gesi hata
hapa Ruvu kwa watani zangu, nako kuna gesi wanalima mpunga juu, lakini
ndani kuna gesi, haiwezekani nchi tajiri yenye gesi kila mahali
tunalalamika masuala ya umeme, tukiwa na umeme wa kutosha hata gharama
zitashuka,” alisema.
Aliongeza: “Kila moja atawasha kwa umeme, hayo ndiyo maisha
tunayoyatafuta Watanzania, Mungu ametupa kila kitu hapa, zipo nchi Ulaya
zinasafirisha gesi kutoka Urusi sisi ipo hapa hapa, haiwezekani
tukaendelea kuwa maskini, lakini na wasomi wapo, iweje tuwe maskini,”
alihoji.
Alisema amepata taarifa mradi wa Kinyerezi I wataongeza megawati 185 na kandarasi anahitaji Dola milioni 20.
“Sasa kama tumetoa milioni 120 (dola) kwa nini tushindwe hizi Dola
milioni 20, mwambie mkandarasi tutazitafuta hata mwezi huu zitapatikana
ili aanze, tunataka umeme uwe kila mahali kwa sababu vyanzo vipo mambo
ya kutumia vyanzo vya umeme vya maji yawezekana wakati wake umepita,”
alisisitiza.
Aliongeza: “Tanzania ina kila kitu hata uranium inaweza kutumika
kama chanzo cha umeme, tuna makaa ya mawe, gesi maji lakini tunalalamika
hakuna umeme na wasomi tumewasomesha, sijui wanaenda kujifunza nini
huko , ndio maana nasema wizara mmenifuraisha, nendeni kwa speed kubwa
zaidi,”alisema.
Alisema ndio maana akasema hachagui mwanasiasa bali mchapakazi kwa sababu maendeleo hayana chama.
“Uwe CUF , Chadema au usiwe na chama wote mnahitaji umeme, ndio
maana nikachagua watu wa kuchapa kazi bila kubagua vyama zao,
nawahakikisha Watanzani serikali yangu itafanya kazi kweli kweli,
mlituchagua bure hatujawahonga, lazima tuwafanyie kazi ili tuondoe kero,
tunawahakikisha bila kigugumizi tumejipanga kufanya kazi,
atakayetukwamisha atakwama yeye na kuondoka ataondoka yeye siku hiyo
hiyo,” alisema.
Alisema Watanzania wamechoka kusubiri kutoka uhuru haiwezekani
waendelee kuwa maskini wakati nchi imebarikiwa na kuwa na rasilimali
kama Tanzanite, bahari, maji , maziwa, dhahabu, almasi na makaa ya
mawe.
“Lazima tutumie nguvu zetu zote, kama tatizo lipo ndani ya
serikali, niachieni mimi nitawanyoosha waliopo ndani ya serikali na
ninyi wananchi isaidieni serikali kwenda mbele wale wanaotaka
kutuchelewesha kwa ajili ya kazi muwapuuze, kila mmoja ajipange kufanya
kazi,” alisema.
KUHUSU FIDIA
Alisema anafahamu wapo waliolipwa fidia Sh. bilioni 30 na wachache ambao hawajalipwa kama Sh. bilioni mbili.
“Tutawaletea hizi fedha mlipwe, lakini wale waliolipwa wasifanye
ujanja ili walipwe tena. Hakuna fedha za bure lazima niwaeleze ukweli
hili siyo shamba la kufanya biashara, tutazileta fedha hizi wapo wawili
walikataa kuzipokea shauri yao, lakini wakitaka kuzipokea waje kuchukua,
wakiona wanataka kwenda mahakamani waende, wale wanaostahili
tutawalipa,” alisema.
Aidha, alimshukuru Balozi wa Japan na Mtendaji Tanesco na kueleza
kuwa mradi upo Kinyerezi kuna vijana na kina mama na wazee wapewe nafasi
ya kwanza kupata ajira hapo.
“Ombi langu vijana mkipata nafasi msiibe vifaa vitakavyotumika
hapa, mjue huu ni mradi wa Watanzania ni wetu sote, tunataka ukamilike
mapema, unapoiba vifaa au mafuta, ujue wewe ni chanzo cha kuchelewesha
maendeleo, mtangulizeni Mungu mbele, ulipwe fedha ili baadaye mradi
uwanufaishe wote,” alisema.
Alisisitiza kuwa maendeleo yataletwa na Watanzania wote kwa
kuwaeleza wana Kinyerezi kuwa anafahamu wana matatizo ya maji, lakini
baada ya umeme kupatikana ndiyo mwanzo mzuri wa kupata maji.