WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekatisha ziara yake ya siku sita
mkoani Simiyu, baada ya kifo cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Maswa (DED), Trasias Kagenzi kilichotokea juzi usiku.
Kaimu Katibu Tawala, Donatus Weginah alithibitisha kutokea kifo cha
mkurugenzi huyo wakati Waziri Mkuu akiwa na ratiba ya kutembelea wilaya
hiyo.
Weginah alisema juzi asubuhi Kagenzi alikuwa akifanya mazoezi ya
kukimbia akiwa na mlinzi wake na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary
Kirigini lakini alianza kujisikia vibaya.
“Mkurugenzi alikuwa akifanya mazoezi ‘jogging’ na DC Rosemary
Kirigini, lakini baadaye alimwambia Kirigini najisikia pumzi zinabana,
akamwambia aendelee… lakini mara mkuu wa wilaya alimuona amejiinamia,
aliporudi kumuuliza akamwambia naona nakosa hewa, ndipo alipoamua
kukimbia kuchukua gari kumpeleka hospitalini,”alisema.
Weginah alisema mkurugenzi huyo alipelekwa hospitali na majira ya saa
tano asubuhi alionekana akiendelea vizuri, hata hivyo baadaye hali
ikabadilika mchana na waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Bugando kwa
uchunguzi zaidi, lakini usiku wa saa saba alifariki dunia.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Tawala huyo, alisema mkurugenzi ana kama
mwaka mmoja na nusu tangu alipohamia wilayani humo na kwamba familia
yake iko Arusha.
Weginah alisema jana mchana mwili wa Kagenzi ulichukuliwa hospitalini
Bugando na kuletwa wilayani Maswa ambapo leo asubuhi Waziri Mkuu
Majaliwa ataongoza kuaga mwili wa mkurugenzi huyo.
Chanzo: Habari Leo