Watu watatu wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakiwa na Bunduki aina ya SMG, wamewaua kwa risasi wakazi wawili wa mtaa wa Bugarika sokoni jijini Mwanza na kuwajeruhi wengine saba baada ya kuvamia kwenye duka la Mfanyabiashara mmoja wa eneo hilo kwa lengo la kupora fedha pamoja na mali mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi Justus Kamugisha amesema tukio hilo limetokea ijumaa machi 25 majira ya saa mbili na dakika tano usiku katika mtaa wa Bugarika sokoni kata ya Pamba wilayani Nyamagana na kuwataja waliouawa kuwa ni Julius Wankaba ambaye ni dereva wa bodaboda aliyepigwa risasi ya kifuani pamoja na Bi. Coletha, maarufu kwa jina la mama Yuni ambaye alipigwa risasi ya shingoni wakati akikimbia kutoka dukani kwake.
 
Aidha Kamanda Kamugisha pia amewataja majeruhi saba wa tukio hilo ambapo wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure na wengine watano wanaoendelea kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Majambazi hao waliovamia dukani kwa Daniel Marwa na kupora fedha taslimu shilingi milioni mbili, vocha zenye thamani ya shilingi laki nane na Simu sita za wateja.

 
Top