Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesisitiza kuwa ataendeleza azma yake ya kuondoa gereji za mitaani, baa na grosari, ikiwa mpango wake wa kusafisha jiji.
Makonda aliyasema hayo alipokuwa akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa
mkuu wa mkoa huo, Saidi Meck Sadiki, ambaye amehamishiwa mkoani
Kilimanjaro.
Mbali na gereji na baa, pia alisema atahakikisha anaondoa yadi za
magari ambazo zimezagaa kila kona ya jiji na kuzihamishia maeneo
maalum.
“Uchafu unaanzia moyoni mwako, nawaomba wananchi kila mmoja asafishe maeneo yao,” alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wa serikali za mtaa wampatie idadi ya wananchi wanaoishi maeneo yao ili kuimarisha ulinzi.
“Nashukuru Rais John Magufuli kwa kunichagua kufanya naye kazi.
Namshukuru baba yangu Meck Sadiki, leo ni siku iliyofungua ukurasa mpya
ambao sikuwahi kuusoma,” alisema.
Sadiki kwa upande wake, alifunguka kwa kusema moja ya changamoto
alizokumbana nazo wakati akiwa Dar es Salaam, ni vuguvugu la uchaguzi
mkuu la mwaka 2010.
Uchaguzi huo ulihusisha wagombea wa vyama vyote wakiwemo Rais
Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete wa CCM na Dk. Willibrod Slaa wa Chadema.
Sadiki ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, aliyasema hayo
jana jijini Dar es Salaam katika sherehe ya kuagwa, iliyohusisha
viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo.
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini wamuunge mkono Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, katika kampeni ya ‘Safisha Jiji Ondoa
Uchafu’.
“Wananchi wa Dar es Salaam ndio wamenifikisha hapa nilipo hadi
Rais (Dk. John) Magufuli alipoamua kunipeleka Kilimanjaro kwenda
kuendeleza mazuri niliyoyafanya hapa,” alisema.
“Nakuombea Makonda ufanye kazi pamoja na kamati ya viongozi wa dini
uwashirikishe katika changamoto utakazokumbana nazo ili wakusaidie
katika kukuombea,” alisema.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgeni rasmi, Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki, Abdulla Ali Hasani Mwinyi, alisema hana tatizo na ungozi wa
Paul Mkaonda kwa kuwa ni kiongozi bora.
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>