Ummmy Mwalimu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Prof.
Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Hatua ya kujiuzulu kwa baadhi ya wabunge wa Kamati ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, ‘kumewaokoa’ mawaziri watatu ‘kuwekwa kikaangoni’
ambao walitakiwa kuhojiwa jana na kamati hiyo.
Wabunge wa Kamati hiyo hawakukutana jana, kutokana na kashfa
inayowaandama ya kupokea rushwa, kitendo kilichosababisha wabunge 12
kutia saini waraka maalum wa kupelekwa kwa Spika, huku wabunge wawili
kati yao wakiandika barua ya kujiuzulu rasmi.
Mawaziri hao ni Ummmy Mwalimu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto), Prof. Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.
Akizungumza na Nipashe jana, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Dk. Raphael Chegeni, alisema kwa siku ya jana, Kamati ilikuwa na
ratiba ya kukutana na mawaziri hao watatu ili kuwahoji mambo mbalimbali
yanayohusu wizara zao.
Alisema kumekuwapo na mkanganyiko au mwingiliano wa utendaji wa kazi kwa wizara hizo tatu.
Alisema katika wizara ya elimu, kumekuwapo na malalamiko ya malipo
ya walimu kwa muda mrefu, hivyo kufanya Tamisemi na Wizara ya elimu
kutupiana mpira katika kutatua kero hiyo.
“ Utakuta matatizo ya malimbikizo ya mishahara ya walimu. Tamisemi
na Wizara zimekuwa zikikwepa majukumu hayo, kila mmoja anadai mwenzake
ndiye mwenye jukumu la kutatua. Tulipanga tuwaite wote kwa pamoja
watueleze,” alisema Dk. Chegeni.
Aliongeza kuwa majukumu ya Wizara ya Elimu na Tamisemi yamekuwa
yakiingiliana na kutoeleweka nani afanye jukumu hili na nani afanye
jukumu lingine.
Alisema kadhalika katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, kumekuwa na mwingiliano wa majukumu baina ya
wizara hiyo na Tamisemi.
Alisema hadi sasa haifahamiki kati ya Tamisemi na Wizara ya afya
nani mwenye jukumu la kusimamia hospitali za rufani, kwa kuwa wizara
zote mbili zimekuwa zikigongana katika kutekeleza majukumu.
Dk. Chegeni alitolea mfano kwa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza,
Magesa Mulongo, Machi 6, mwaka huu, alipowasimamisha kazi madaktari
wawili na wauguzi watano wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou
Toure kutokana na uzembe unaodaiwa kusababisha kifo cha mama mzazi Pendo
Masanja na watoto wake mapacha.
Dk. Chegeni alisema kitendo hicho hakikuwa sahihi kwa kuwa mkuu wa
mkoa hakuwa na mamlaka ya kuwasimamisha kazi madaktari hao na waguzi
wakati Wizara ya afya ipo na ndiyo yenye jukumu la kuwachukulia hatua
madaktari hao na wauguzi.