Mbali na matarajio hayo ya wananchi, kauli za viongozi wa Ukawa
kusema kuwa kuna ufisadi kwenye mikataba mbalimbali ukiwamo ule wa
Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (Uda), zabuni mbalimbali zikiwamo
za kusomba taka, upangishaji nyumba za Jiji na kuuza maeneo ya wazi, ni
kati ya mambo ambayo yanatarajiwa kupatiwa ufumbuzi.
Kadhalika, baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa vikizua maswali mengi
juu ya uhalisia wake ni pamoja na makusanyo ya mapato mbalimbali kama ya
Soko la Kariakoo.
Licha ya soko hilo kuwa na wafanyabiashara wengi, imeelezwa kuwa
linakusanya wastani wa Sh. milioni 180 kwa mwezi kutoka kwa wazabuni
wanaokusanya mapato, hali inayoonyesha kuwa bado soko hilo linakusanya
fedha kidogo kinyume cha matarajio ya serikali.
Pia, fedha zitokanazo na mabango, ni kitendawili kingine ambacho
licha ya kuwapo kwa mabango ya matangazo, inaelezwa kuwa fedha nyingi
huingia kwenye mifuko ya wajanja.
Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob, Februari 16, mwaka huu,
aliwaleeza waandishi wa habari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni imekuwa ikipoteza Sh. bilioni 11 kila mwaka kutoka katika
vyanzo vya mapato vya mabango makubwa ya matangazo.
Alisema upotevu wa fedha hizo ulikuwa ukitokea kila mwaka kupitia
kampuni 12 za matangazo makubwa ambazo hushirikiana na watumishi wa
manispaa hiyo.
Alisema tangu alipoingia katika uongozi wa manispaa hiyo, wamebaini
udanganyifu mkubwa uliokuwa unafanywa na walipa ushuru, jambo
lililosababisha kufanya utafiti.
“Hapo awali Manispaa katika vyanzo vyake vya mapato kupitia ushuru
wa mabango, tulikuwa tukikusanya Sh. bilioni 2.5 kwa mwaka, lakini
tulikuwa tukilaumiwa kwa kukusanya kiasi kidogo, ila kwa sasa tumegundua
katika ukusanyaji huo hata robo tulikuwa hatufikii,” alisema na
kuongeza:
“Hayo mabango mnayoyaona barabarani yalikuwa na udanganyifu wa
vipimo pamoja na idadi kwa kila kampuni, tumepitia mabango yote katika
manispaa hii na idadi yote tunayo na tumeyapima upana pamoja na urefu,
tumegundua tulikuwa tukipoteza zaidi ya Sh. bilioni 11.5 kwa mabango
makubwa na kwa kampuni za mabango madogo tulikuwa tunapoteza Sh. milioni
662.”
Wakati danadana za kumpata Meya wa Jiji zikiendelea, Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliwahi
kunukuliwa na vyombo vya habari akisema:
“Hii ni mikakati ya makusudi ya wenzetu wa CCM na serikali kuficha
ufisadi ambao umefanyika ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Wanaogopa
viongozi kutoka upinzani watakwenda kuyatibua.
“Kuna ufisadi mkubwa wa (Uda), viwanja vya Jiji na kuna wizi mkubwa
wa kandarasi jijini. “Tuna taarifa juu ya maandalizi ya kuvunja baraza
la madiwani ili kuundwa tume itakayoongoza Jiji la Dar es Salaam. Mpaka
sasa umefanyika mkakati wa makusudi wa kuigawa Manispaa ya Ilala na
Kinondoni ili kuvunja nguvu ya Ukawa.”
Mbali na Mbowe, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jacob, naye
alinukuliwa akisema: “Katika halmashauri hizi, CCM wana maslahi mapana,
kuna mikataba hewa ambayo ilikuwa ikiwanufaisha wao siyo manispaa.
Wanajua tukiingia tutaweka wazi kila kitu pamoja na kufuta mikataba
hiyo.”
Kashfa ya uuzwaji wa Uda ambayo inahusishwa na vigogo wa CCM,
imewahi kufikishwa katika Bunge la 10 ingawa iliyeyuka katika mazingira
ya kutatanisha.
Kashfa hiyo pia iliyokuwa imeshikiwa bango na wabunge wa CCM,
ilifanya wa chama hicho na madiwani kukosoana, hatua iliyofanya
aliyekuwa Meya wa Jiji, Dk. Didas Massaburi, kuwaambia wanafikiria kwa
kutumia 'makalio'.
Jana, Meya wa Kinondoni, Jacob aliliambia gazeti hili kuwa kuna
madudu mengi ambayo wameyagundua tangu waingie madarakani, lakini kwa
sasa ni mapema kuyasema.
“Huwezi ukaweka kila kitu hadharani sasa hivi, muda ukifika kila
kitu kitakuwa hadharani, lakini ni madudu mengi tumeyagundua na
tutayatumbua tu,” alisema Jacob.
Juzi baada ya kuchaguliwa, Meya wa Jiji Isaya Mwita, alisema baadhi
ya mambo atakayoshughulikia kwenye uongozi wake ni changamoto ya
foleni.
Pia, uchafu ambao alisema Jiji la Dar es Salaam likilinganishwa na
mengine ya Afrika Mashariki, linaongoza kwa uchafu, ambalo nalo
atalishughulikia.
“Kuna tatizo la bodaboda, nafahamu kilio chao, mama ntilie hawana
maeneo, lakini wale wanaoishi mabondeni nitaangalia namna gani ya
kuwezesha waendelee kuishi Dar es Salaam,” alisema.
Alisisitiza kuwa Jiji halitaendelea endapo migogoro ya muda mrefu ya kiitikadi haitaisha.
“Nataka kuona si CCM, Chadema au CUF, bila kujali itikadi za vyama
vyao, wote tunafanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Hii ni mara ya kwanza Jiji hili linashikiliwa na upinzani, kwa hiyo kazi
kubwa niliyonayo ni kuhakikisha miaka mitano ijayo maendeleo
yanapatikana. Nawaomba wananchi watupe ushirikiano,” alisema.
Chanzo: Nipashe