Chanzo cha ajali iliyotokea Tabata Matumbi jijini Dar es Salaam
Jumatano na kuua watu wanne na 26 kujeruhiwa, kimefahamika baada ya majeruhia
kuelezea mwanzo mwisho wa tukio hilo.
Akizungumza na Nipashe jana akiwa Hospitali ya Amana, Jane Ngama,
ambaye alidai kuumia nyonga, alisema kisa cha ajali hiyo ni mwendo kasi
wa daladala hiyo ambayo ilikuwa ikitoka Gongo la Mboto kuelekea Ubungo.
Alisema ajali hiyo ambayo ilitokea majira ya saa 11 alfajiri,
ilihusisha magari matatu ikiwamo daladala hiyo ambayo ilibeba abiria na
kisha kugonga lori la mchanga kwa nyuma kabla ya kubadilisha mwelekeo na
kwenda upande wa pili kisha kugongwa lori lingine.
Alisema daladala hiyo yenye namba za usajili T629 CRT aina ya DCM,
baada ya kubadili mwelekeo, ilihamia upande wa pili wa barabara kama
inaelekea Buguruni kisha kugongwa tena na lori lililokuwa limebeba
ng'ombe.
Alisema licha ya daladala hiyo kuwa katika mwendo kasi, hata lori hilo la mchanga nalo likuwa katika mwendo kasi.
Jane alisema kama madereva hao wangekuwa kwenye mwendo wa kawaida
isingetokea ajali kubwa kama hiyo iliyowasababishia majeraha na baadhi
kupoteza maisha.
Ngama ambaye ni Katibu Muktasi katika Halmashauri ya Kibaha,
alisema hulazimika kuondoka alfajiri ili kuwahi kazini, lakini jana hali
ilikuwa tofauti baada ya safari yake kuishia njiani kutokana na kupata
ajali.
“Ilikuwa niwahi Ubungo ili nichukue daladala ya kuwahi kazini
kwangu Kibaha, ndipo nikakutana na ajali, nina kila sababu ya kumshukuru
Mungu maana hii ajali ilikuwa ni ya aina yake, Mungu ameweka mkono
wake, sikutegemea kama ningekuwa hivi nilivyo,” alisema.
Aidha, alishukuru kwa huduma alizopatiwa katika Hospitali ya Amana kwani wamejitahidi katika kuhakikisha wanapatiwa huduma bora.
“Nimejulishwa napatiwa rufani ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuwa nyonga imeachia,” alisema Jane.
Naye Willins Lyimo ambaye alijeruhiliwa maeneo mbalimbali ya mwili
wake, hatua iliyomsababishia kushindwa kutembea kutembea, alisema ajali
hiyo imesababishwa na dereva wa lori ambaye alitaka kukata kona bila
kutoa taarifa hivyo kuigonga daladala hiyo.
Alisema lori hilo lisingekuwa kwenye mwendokasi kungekuwa na
uwezekano wa kutokea ajali ndogo ambayo isingekuwa na madhara kwa
binadamu.
“Nilichokiona ni huyu dereva wa lori la mchanga hakuonyesha alama
kama anataka kukata kona, matokeo yake akaigonga daladala baada ya hapo
sikujua kilichoendelea, nilijikuta nipo chini sijajua kama tuligongwa
tena maana nilikuwa nimekaa siti za mbele,” alisema Lyimo.
Hata hivyo, Lyimo alisema alipanda daladala hiyo kwa lengo la
kuelekea Stendi ya Mabasi ya Mikoani ili apate usafiri wa kuelekea Mkoa
wa Kilimanjaro kwa ajili ya kushughulikia matatizo yake ya kifamilia.
Akizungumzia na Nipashe kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Ilala, Lucas Mkondya, alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11
alfajiri baada ya daladala ya abiri kugongwa na lori la mchanga.
“Lori la mchanga lilikuwa nyuma ya daladala hiyo na kuigonga kwa
nyuma, hivyo kuhamia upande wa pili wa barabara ya kuelekea Buguruni
kisha ikagongwa tena kwa mara ya pili na lori lililokuwa limebeba
ng’ombe,” alisema Kamanda Mkondya.
Kamanda Mkondya alisema katika ajali hiyo watu wanne wamepoteza
maisha akiwamo dereva wa daladala na kwamba, majeruhi ni 26, huku
daladala hiyo ikiharibika vibaya.
Aidha, kamanda huyo alisema chanzo cha ajali hiyo katika uchunguzi
wao wa awali, wamebaini kuwa dereva wa lori alikuwa kwenye mwendo kasi
na kwamba amekimbia na wanaendelea kumtafuta ili achukuliwe hatua kwa
mujibu wa sheria.
Alisema maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Amana na majeruhi
walifikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Naye Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Stanley Binagi, alisema walipokea maiti tatu na majeruhi 26.
“Kati ya majeruhi hao, mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu
hivyo idadi ya vifo ikaongezeka na majeruhi kupungua na kufikia 25, na
watano kati ya hao wamepelekwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili
ya huduma zaidi pamoja na kufanyiwa uchunguzi kwa kuwa hali zao hazikuwa
nzuri,” alisema.
Aliwataja majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kuwa ni Victoria
Msangi, Neema Kimario, Janeth Mwakyusa, Bakari Jafari, Rabia Omary,
Amina Ridhiwani, Lisrea Daud, Jane African, Venance Iliaeli, Wilence
Lyimo, Samiat Salim, Rozalia Malawaiya, Gasper John na Jane Ngama
Wengine ni Jumanne Simon, Deo Kimario, Eliseli Lyimo Stephano Tibu,
Didas Lucas, Yasini Abdallah, Said Hussein, Abas Nassoro, Salim Bashir,
Hussein Yunus na Mwanaasha Ramadhani.
Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Muhimbili, Neema Mwangomo,
alithibitisha kuwapokea majeruhi saba ambapo kati ya hao watatu
wamehamishiwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi).
Chanzo: Nipashe