BODI ya Sukari Tanzania imeshusha bei ya sukari kwa kutangaza bei
elekezi, inayoonesha bidhaa hiyo kuanzia sasa inauzwa Sh 1,800 kwa kilo
nchini kote. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi, Henry Simwanza alisema, wafanyabiashara wote wanapaswa
kuzingatia agizo hilo.
Aidha alisisitiza wafanyabiashara kuhakikisha kuwa sukari inaendelea
kusambazwa na kuuzwa kwa wananchi bila kuihodhi. Awali, juzi
alipozungumza na waandishi wa habari, Simwanza alisema bei elekezi ya
sukari ilikuwa Sh 2,000 kwa Dar es Salaam na miji jirani.
Kwa upande wa mikoa iliyo pembezoni, bei ilielekezwa iwe 2,200. Hata
hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema juzi wakati
akisisitiza bei elekezi hiyo (ya awali), kulikuwa na kikao kingine
kikiendelea kujadili suala la sukari, ambacho ndicho kilifikia uamuzi wa
bei ya Sh 1,800 baada ya kujiridhisha.
“Kuhodhi bidhaa ni kuhujumu uchumi wa nchi, sukari ni bidhaa nyeti
inayohitajika sana. Tunawataka wafanyabiashara wote watii agizo hili,”
alisema Simwanza. Alisema maofisa wa bodi ya sukari Tanzania, kwa
kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali, hususani maofisa biashara
wa mikoa na wilaya watafuatilia na kusimamia utekelezaji wa agizo hilo
la bei elekezi.
“Serikali ikisema kitu ni amri. Niseme tu hatutasita kuchukua hatua
stahiki za kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei au kuhodhi
bidhaa hiyo,” alisema Simwanza. Juzi Simwanza akizungumza na vyombo vya
habari alisema upatikanaji wa sukari nchini ni wa kuridhisha na ipo
akiba ya kutosheleza nchi nzima.
Alisema pamoja na baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji wa sukari
kutokana na msimu kuisha, hali ya bidhaa hiyo nchini ni nzuri na ipo
zaidi ya tani 62,000. Aliwataka wasambazaji wakubwa wa sukari hususani
kampuni ya Alneen Enterprise ya jijii Dar es Salaam , ambayo
imethibitisha kuwa na sukari tani 8,600, waitoe na kuiuza.
Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles
Mwijage alisisitiza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na kuwataka
wafanyabiashara walio na leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo,
kutoificha.
Mwijage alitaka watu wenye taarifa juu ya mfanyabiashara aliyefungia
sukari katika ghala lake ampelekee, afunge ghala husika mara moja.
Alisema serikali inajikita zaidi katika uanzishaji wa viwanda vya sukari
na kuongeza ajira na si katika kuagiza sukari kutoka nje.
Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na mazungumzo inayofanya na
mwekezaji anayetaka kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha sukari mkoani
Kigoma, atakayewasili nchini wakati wowote kukamilisha taratibu.
Chanzo: HabariLeo