Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Mkuranga, Thobias Mapalala, amejeruhiwa baada ya kuchomwa mkuki mkononi wakati wa operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa mashamba wilayani humo.

OCD Mapalala alikimbizwa hospitali baada ya tukio hilo, alipokuwa kwenye operesheni iliyowahusisha askari kutoka Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani na wa Wilaya ya Mkuranga.

Operesheni hiyo iliyoanza juzi ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza la kuwaondoa mamia ya vijana waliovamia mashamba yaliyoko kwenye kitongoji cha Mkoga na Mkombozi.

Akizungumza na Nipashe jana, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Ali Mtamilwa, alisema OCD alijeruhiwa jana mchana wakati wa mapambano ya kuwaondoa vijana hao.

“Tulikuwa kwenye harakati za kuwakamata vijana hao waliovamia mashamba, mmoja wao aligoma kutoka ndani ya nyumba yake na afande alipokaribia pale ili kufungua mlango wake, alichomoa mkuki na kutaka kumchoma nao," alisema Mtamilwa.

"Katika kujihami afande aliupangua mkuki huo kwa mkono na ndipo ulipomchana mkononi.”

Mtamilwa alisema baada ya OCD kuchomwa mkuki, askari walianza kurusha mabomu ya machozi ndipo mtuhumiwa huyo alipotoka mbio ndani ya nyumba yake akijaribu kuwakwepa lakini alikamatwa.

Mtamilwa ambaye ni diwani wa Kata ya Tambani Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, alisema OCD alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu wakati zoezi hilo likiendelea chini ya askari wengine waliokuwa wakisimamia zoezi hilo.

Vijana hao wanaotokea Kitunda, Msongola na Chamazi mkoani Dar es Salaam wamejitengenezea serikali yao, alisema Mtamilwa na kubainisha kuwa wamekuwa wakivamia watu na kuwahamisha kwa nguvu kisha kuweka makazi yao ya kudumu.

“Raia wa kawaida huwezi ukaja huku peke yako maana sidhani kama utarudi salama, fikiria sisi tumekuja na askari wa kutosha lakini wameleta vurugu na hadi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatia nguvuni,” alisema diwani huyo.

Alisema pamoja na kuonyesha upinzani, lakini polisi walifanikiwa kuwakamata vijana 18 akiwemo aliyemjeruhi OCD, ambaye naye alijeruhiwa kwa bati la mlango wa nyumba yake akiwa katika harakati za kukimbia.

Alisema vijana hao wamekuwa wakivamia mashamba ya watu na kujenga makazi ya kudumu na wakati mwingine kuyauza kwa watu wengine kwa kutumia hati za kughushi.

“Wanachofanya hawa watu ni kama ujambazi maana wakiwakuta watu huku wanawatisha tisha na kuhakikisha wanahama," alisema na kueleza zaidi, "wanawafanya watu wanaowakuta waishi kwa hofu mpaka wanakimbia wenyewe wanakuwa wengi sana.

“Mwenyeji akikimbia wanachukua kila wanachokiona, kama umeacha matofali, mbao na hata mabati wanang’oa wanaondoka nayo kwenda kuyatumia kwenye nyumba zao, yaani ni kama walijijengea ufalme wao lakini safari hii watahama wao maana operesheni hii ni kubwa.”

Alisema RC aliagiza operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao iwe imekamilika kwa siku tatu, muda ambao alisema anaamini watakuwa wamefanikiwa kuwaondoa.

Alipotafutwa na gazeti hili, Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Pwani, Boniventula Mushongi, alithibitisha tukio hilo lakini akashindwa kutoa ufafanuzi zaidi kwa sababu "niko kwenye msafara wa Rais (John Magufuli) kwenye msiba huku Bagamoyo."

Rais Magufuli alikuwa Bagamoyo kuhani msiba wa kaka wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete mkoani Pwan.
Chanzo: Nipashe

 
Top