INAWEZA kuwa fungu la kukosa kwa Simba baada ya kupoteza kwa bao 1-0
mechi dhidi ya Toto Africans na hivyo kutia ugumu mbio zake za kuwania
ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilihitaji ushindi katika mechi hiyo ya jana ili kulingana pointi na Yanga kwenye mbio za ubingwa.
Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 59 na Simba ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 57.
Ni fungu la kukosa kwa Simba baada ya kutolewa kwenye michuano ya
kombe la Shirikisho na hivyo nafasi pekee ya timu hiyo kushiriki kwenye
michuano ya kimataifa kubaki kwenye Ligi Kuu.
Toto Africans ilipata bao lake katika dakika ya 20 likifungwa na
Waziri Junior aliyeunganisha pasi ya Edward Christopher na kupiga shuti
kali akiwa nje ya 18 na mpira kujaa wavuni.
Simba sasa ina kazi ya ziada kuifukuzia Yanga katika mbio hizo za
ubingwa, jambo ambalo linaonekana gumu kutokana na ubora wa Yanga.
Pamoja na bao hilo la kipindi cha kwanza, Simba bado walionekana kutawala mchezo huo hasa kwenye kipindi cha kwanza.
Mechi hiyo ilizidi kuwa mbaya kwa Simba pale mwamuzi Ahmad Simba
alipomtoa kwenye benchi kocha Jackson Mayanja baada ya kumfokea dakika
ya 30.
Dakika saba baadae, Hassan Kessy alishindwa kuisawazishia Simba bao
akiwa amebaki pekee na kipa wa Toto lakini shuti lake lilipanguliwa.
Kipindi cha pili kilianza vibaya kwa Simba baada ya mwamuzi Simba
kumtoa Kessy kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Christopher katika
dakika ya 47.
Baada ya mechi hiyo, mashabiki wa Simba walimfuata Mwenyekiti wa
kamati ya usajili, Zacharia Hanspoppe na kumlaumu kwa kusajili timu
mbaya isiyo na wachezaji wenye uwezo.
Mashabiki hao walimrushia Hanspoppe michanga jambo lililomfanya
kushindwa kuvumilia na kuingia ndani ya gari yake ambapo alitoa bastola
kiunoni na kuiweka kwenye kiti kisha kuendesha gari kwa kasi.