MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan leo atawasha Mwenge wa Uhuru na
kuzindua rasmi mbio zake ili kukimbizwa katika halmashauri za wilaya na
Manispaa zipatazo 179 za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani.
Uzinduzi huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
ambao utatanguliwa na shamrashamra za halaiki kutoka kwa vijana zaidi ya
1,000 na vikundi vya utamaduni kutoka wilaya za Morogoro na nje ya mkoa
huo.
Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na vyama
vya siasa wamealikwa kushiriki wakiwemo pia mawaziri wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
Miongoni mwa mawaziri ambao hadi jana walikuwa tayari wamewasili
mkoani hapa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Bunge, Sera, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama na Waziri wa
Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Mouldine Castico.
Mawaziri hao jana waliungana na Makamu wa Rais kutembelea mradi wa
vijana wajasiriamali wa mafundi seremala eneo la Mtaa wa Betero, Kata ya
Sabasaba, Manispaa ya Morogoro. Kaulimbiu za Mwenge wa Uhuru mwaka huu
ni “Vijana ni Nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na Kuwezeshwa.”
Baada ya kuwashwa leo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri
ya Manispaa ya Morogoro na kuhitimishwa wilayani Gairo ambako Aprili
25, mwaka huu utakabidhiwa mpakani mwa wilaya hiyo na Kilindi ya Mkoa wa
Tanga ili kuendelea na mbio zake.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu,
utakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa zipatazo 179 na kilele cha
mbio hizo ni Oktoba 14, mwaka huu katika Mkoa wa Simiyu.
Mwenge wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza Desemba 9, 1961 kwenye
kilele cha mlima Kilimanjaro, kutimiza ahadi ya Rais wa Kwanza wa
Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai Uhuru wa Tanganyika.