MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameahidi kutoa zawadi ya
fedha kwa mwalimu atakayefaulisha mwanafunzi katika somo lake la
sayansi, lengo likiwa ni kutoa motisha kwa walimu.
Makonda aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizindua programu
ya kuwasaidia wanafunzi waliotoka katika familia masikini iliyoandaliwa
na shule za Feza.
Feza wametoa Sh milioni 37.5 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi 150 wanaotoka katika familia masikini.
Makonda alisema atatoa Sh milioni 15 kwa mwalimu wa sekondari
atakayefaulisha mwanafunzi katika masomo ya Sayansi na Sh milioni 10 kwa
mwalimu wa kidato cha pili atakayefaulisha mwanafunzi katika masomo ya
sayansi na Sh milioni tano kwa mwalimu wa shule ya msingi
atakayefaulisha mwanafunzi.
“Niseme sitaishia kwenye kutoa fedha pekee, mwalimu huyo na familia
yake watachagua mbuga yoyote ya wanyama watakayoitaka na nitagharamia
kila kitu, naamini kwa kufanya hivyo kutajenga motisha hata kwa walimu
wengine kuongeza jitihada na kuhakikisha anafaulisha wanafunzi,” alisema
Makonda.
Aidha, Makonda amewashukuru Feza kwa kuamua kuwasaidia wanafunzi hao
na amewataka wazazi kuhakikisha wanasimamia vyema fedha hizo ili zifanye
kazi iliyokusuduwa.
“Sitopenda kusikia mama ametumia fedha hizo tofauti na nyinyi
wanafunzi muwalipe wafadhili hawa kwa kusoma kwa bidii, hakuna mtu
atakubali kuendelea kutoa msaada kwa mtu ambaye haoneshi juhudi,”
aliongeza Makonda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule hizo, Isa Otcu alisema shule
hizo zimeamua kutoa msaada huo kwa ajili ya kumuunga mkono Rais John
Magufuli katika harakati zake za elimu bure.
Alisema programu hiyo itatoa kiasi cha Sh 250,000 kwa kila mwanafunzi
na tayari wameshaweka kiasi cha Sh 100,000 katika akaunti za wanafunzi
hao kuanzia Januari mpaka Aprili.
Aliongeza kuwa wameamua kuwateua kina mama kwa ajili ya kusimamia
fedha hizo ambazo zitawekwa katika akaunti zao za benki, kwani wanaamini
mama ana uwezo wa kuhifadhi kwa faida ya watoto wake.