KAMATI maalumu ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda imefichua madudu na harufu ya ufisadi katika
utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato
ya Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji
magari katikati ya mji.
Kutokana na madudu hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha wazi kuwa
hataki kufanya kazi tena na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson
Kabwe na Kaimu wake, Sarah Yohana na kuwasilisha majina yao kwa mamlaka
husika ya nidhamu kwa hatua zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema hivi
karibuni aliunda kamati hiyo maalumu kufuatilia maeneo hayo muhimu
kutokana na malalamiko ya muda mrefu, ambayo ofisi yake ilikuwa ikipokea
kutoka kwa wananchi.
Alisema kwa mujibu wa uchunguzi, kamati hiyo ilibaini kuwa katika
stendi ya mabasi ya Ubungo, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za
umma, ikiwemo kutokuwasilishwa kwa mapato halisi yanayotokana na
makusanyo ya kila siku serikalini.
“Kamati ile imebaini kuwa pale ubungo kunatumika sheria ndogo mbili
za ukusanyaji mapato moja ya mwaka 2004 na nyingine mwaka 2009 kwa lengo
la kunufaisha wachache,” alisema Makonda.
Alifafanua kuwa Sheria Ndogo ya Mwaka 2004 ya ukusanyaji mapato ndani
ya kituo hicho, inaonesha kuwa kila basi linatakiwa kutozwa Sh 4,000,
hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na mabasi 350
yanayoegeshwa kituoni hapo.
Hata hivyo, alisema kutokana na mabadiliko ya tozo, sheria hiyo
ilibadilishwa mwaka 2009 na kila basi likawa linatozwa Sh 8,000 na hivyo
makusanyo ya mwezi yakapanda na kufikia Sh milioni 82 kwa mwezi.
“Lakini cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni inayokusanya
mapato katika kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa kutumia
sheria ya mwaka 2004 yaani Sh milioni 42 badala ya Sh milioni 82 kwa
mwezi…” “…Mbaya zaidi kamati ile katika ukaguzi wake, ilikuta kampuni ya
ukusanyaji mapato hayo stendi ya Ubungo inayo Sheria ya Mwaka 2009
lakini katika nyaraka za Halmashauri ya Jiji zinaonesha sheria
inayotumika ni ya mwaka 2004,” alisisitiza Makonda.
Alisema katika uchunguzi ilibainika kuwa kampuni iliyo chini ya
Halmashauri ya Jiji inayokusanya mapato hayo stendi ya Ubungo, ilisaini
mkataba wa ukusanyaji mapato hayo kwa mara ya kwanza Januari 31, 2004 na
baadaye ikasaini tena mkataba Januari 30, mwaka jana.
Kwa mujibu wa Makonda, kwa hali ilivyo tangu Sheria Ndogo ya Mwaka
2009 ipitishwe, haijawahi kutumika na hivyo kulisababishia hasara jiji
hilo ya Sh bilioni tatu kutokana na mapato katika stendi hiyo kuendelea
kuwasilishwa kwa kutumia sheria ya mwaka 2004.
“Ukipiga hesabu za harakaharaka utagundua kuwa kila mwezi Sh milioni
42 zimekuwa zikipotelea kwenye mikono ya wachache, kwa maana hiyo
kuanzia mwaka 2009 Sh bilioni tatu zimepotea na kila mwaka tumekuwa
tukipoteza Sh milioni 500, huu ni ufisadi wa aina yake kwa kweli,”
alisema.
Alisema wakati fedha hizo zikipotea kwenye mikono ya wachache, kamati
hiyo pia ilibaini kuwa hali ni mbaya katika kituo hicho cha Ubungo
kwani pamoja na ukosefu wa vyoo na maegesho bora kwa mabasi, lakini pia
vibanda vya biashara vilivyomo ndani ya stendi hiyo, vimekuwa vikitumika
kukandamiza maskini na kunufaisha wachache.
“Kwa mujibu wa taratibu, kila kibanda mle ndani ya stendi kinatakiwa
kukodishwa kwa Sh 200,000 kwa mwezi, lakini tumebaini kuwa wapo watu
wachache wamevihodhi na kuvikodisha kwa zaidi ya Sh milioni 1.5,”
alisema.
Kuhusu mkataba wa maegesho katikati ya jiji kupitia Kampuni ya
National Parking System (NPS), alisema kamati hiyo pia imebaini kuwa
Halmashauri ya Jiji imeiongezea mkataba wa miezi 10 kampuni hiyo kinyume
cha taratibu wakati mkataba wake ulikuwa umeshamalizika.
Alisema mara baada ya mkataba huo kumalizika Agosti mwaka jana
Mkurugenzi wa Jiji, Kabwe aliiandikia barua kampuni hiyo na kuiongezea
muda wa miezi sita kwa madai kuwa mchakato wa kutafuta mzabuni mpya
pamoja na kwamba umeanza, haujakamilika.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Yohana naye aliandika miezi kadhaa baadaye
barua na kuiongezea tena kampuni hiyo muda wa miezi minne iendelee
kukusanya kodi ya maegesho kwa kuwa bado mchakato wa kutafuta mzabuni
mpya haujakamilika.
“Barua zote mbili zina saini ya viongozi hawa wawili, hatua hizi ni
kinyume kabisa na maadili ya viongozi pamoja na Katiba ya nchi.
Haiwezekani mchakato wa kumtafuta zabuni uchukue zaidi ya miezi sita,”
alieleza Makonda.
Pamoja na hayo, Makonda pia alisema kamati hiyo katika uchunguzi wake
dhidi ya Kampuni ya Tambaza inayosimamia makosa ya pikipiki na maegesho
ya magari katika sehemu zisizotakiwa, imekuwa ikitoza fedha nyingi za
faini kinyume cha mkataba.
“Mkataba wao unaonesha wazi kuwa wanatakiwa wakikamata pikipiki yenye
makosa watoze faini ya Sh 20,000 lakini imebainika wao wanatoza zaidi
ya Sh 80,000. Licha hivyo pia mkataba unawataka wazingatie dharura na
kutotumia lugha chafu lakini yote haya hawayazingatii,” alisema.
Alisema tangu Rais John Magufuli aingie madarakani amekuwa mstari wa
mbele kupiga vita ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na ufisadi hivyo
akiwa kama Msaidizi wa Rais anaunga mkono juhudi hizo ndio maana hawezi
kunyamazia madudu yeoyote yanayohusu ufisadi.
“Nimewasiliana na mamlaka husika ya nidhamu ili ichukue hatua stahiki
dhidi ya viongozi hawa wawili Kabwe na Yohana na nimeiambia mamlaka hii
kwa uwazi kabisa siwahitaji kuendelea nao hapa Dar es Salaam,”
alisisitiza.
Aidha, alisema tayari amewasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) kuhusu mikataba hiyo yote mitatu ambayo imeahidi
kuanza kuifanyia kazi leo.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuwashughulikia wakurugenzi
hao kwa kuwa wao ndio tatizo kwani mikataba hiyo hata ikivunjwa kwa sasa
itakuwa ni kazi bure kama viongozi hao wataendelea kuwepo.
Hii ni mara ya pili kwa Stendi ya Ubungo kuingia katika kashfa ya
ubadhirifu wa fedha, ambapo mwaka 2011, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo
Pinda aliagiza ufanyike uchunguzi, uliobaini kuwepo kwa madudu, hali
iliyosababisha mzabuni aliyekuwepo kuondolewa.